Mbunge wa Kilwa Kusini, Suleiman Bungara maarufu Bwege, (CUF), amesema alifuatwa ili akubali kununuliwa kwa kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM), akakataa.
Bwege amesema hayo jana Alhamisi Novemba 8, bungeni jijini Dodoma, wakati akichangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa 2019/20, ambapo alisema kwenye kitabu cha Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango, zinaonyesha fedha nyingi za miradi ya maendeleo hazikupatikana, lakini bado nyingine zinatumika kununua watu na chaguzi ndogo zisizo na sababu.
Kauli hiyo ilifanya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama, kusimama na kuomba mwongozo akidai kauli za Bwege kuwa ilani imeshindwa kutekelezwa kwa kuwa fedha zote zimeenda kununua watu si kweli, na inavunja kanuni za Bunge.
Bwege alipopewa nafasi ya kuendelea na mchango wake, alisema yeye anazungumzia chaguzi ndogo zinazofanyika nchini ambazo hazina tija.
“Mimi mwenyewe walinifuata ili waninunue lakini nikakataa, naweza kutaja hata ni nani na nani walinifuata.”
Kauli hiyo ilimfanya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kusimama na kusema; “Mheshimiwa Bungara ukiingia kwenye anga zangu nikakuambia uthibitishe sijui itakuwaje…”
Baada ya onyo hilo Bwege alisema “haya mzee mwenzangu,” akimaanisha Spika Ndugai.
Katika hatua nyingine, Bwege alimshangaa Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Kangi Lugola, kudai kuwa polisi hawaui watu na kuongeza kuwa ana ushahidi wa watu wake waliouawa wakiwa msikitini na alishafikisha suala hilo hadi kwa Waziri Mkuu.
“Nilimleta baba mzazi wa mtu aliyeuawa na polisi na aliyetolewa jicho, Waziri Mkuu mwenyewe alisema Serikali imekosea,” alisema Bwege.