Shirikisho la soka barani Afrika (CAF) kupitia kamati yake inayoshughulika na kuandaa Tuzo za CAF 2018, imeweka wazi vigezo vya wachezaji watakaochaguliwa kuwania tuzo mbalimbali mwaka huu huku moja ya vigezo vikonekana kumpa nafasi nahodha wa Tanzania Mbwana Samatta.
Kamati hiyo imesema kigezo kikuu kitakachotumika kuchagua washiriki wa tuzo ni kiwango cha muhusika kuanzia mwezi Februari 2018 hadi Novemba 2018. Kigezo hiki hakijamtenga sana nyota huyo wa KRC Genk, kutokana na kuonesha kiwango bora katika kipindi hicho kilichotajwa.
Tangu msimu wa 2018/19 uanze katika ligi kuu ya Ubelgiji tayari Samatta amefanikiwa kufunga mabao 10, akiwa kinara wa mabao kwenye ligi hiyo huku pia akiwa ameshafunga mabao 3 katika michuano ya kombe la Europa.
Samatta tayari ni mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani, tuzo ambayo aliipata wakati akiichezea TP-Mazembe msimu wa 2015/16 ambapo aliibuka mfungaji bora wa ligi ya mabingwa Afrika kwa kufunga mabao 7.
Tuzo hizo ambazo hutambua na kuheshimu wachezaji, viongozi na watendaji wengine ambao wamefanya vizuri mwaka huu, zitatolewa Jumanne, Januari 8, 2019 huko Dakar, Senegal.
Vipengele vitakavyowaniwa.
1. Mchezaji wa Afrika wa Mwaka
2. Mchezaji bora wa Wanawake wa Mwaka
3. Mchezaji bora kijana wa Mwaka
4. Kocha bora wa Wanaume wa Mwaka
5. Kocha bora wa Wanawake wa Mwaka
6. Timu bora ya taifa ya Wanaume
7. Timu bora ya taifa ya Wanawake
8. Goli bora la Mwaka
9. Kikosi bora cha Afrika 'First XI'
10. Tuzo ya Rais wa CAF
11. Tuzo ya Platinum