Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kimetetea hatua ya Mbunge wake wa Jimbo la Ndanda, Cecil Mwambe kuingia na ilani ya Chama Cha Mapinduzi bungeni kwa kile ilichokisema kuwa ni jambo la kawaida.
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje CHADEMA, John Mrema amewataka watu wasishangae kwani chama hicho kinawahamasisha wabunge wake kusoma ilani ya CCM ili kujua namna gani ambavyo chama hicho tawala kinatekeleza ilani ahadi.
"Ni jambo la kawaida sana, sababu sisi kama chama tunahamasisha wabunge wetu kusoma, ndio maana huyo huyo Mwambe wiki iliyopita ulimuona anampa sera mbadala za Chama moja ya mawaziri Bungeni," amesema Mrema.
Aidha amesema "kuingia na ilani ya Chama Cha Mapinduzi sio tatizo kwa sababu hata ukija ofisini kwetu utakutana na ilani ya CCM kwa hiyo kama angekuwa na nia ya kuhama chama, angehama kimya kimya kama wanavyofanya wengine".
Leo Novemba 14, 2018 akiongoza vikao vya bunge, Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson amesema "mheshimiwa Cecil Mwambe anasoma sana ilani ya Chama Cha Mapinduzi, siku hizi baada ya kugundua ina mambo mazuri sana".