Jeshi la polisi mkoani Dodoma linamshikilia Hassan Abdalah mkazi wa Wilaya ya Gairo, mkoani Morogoro kwa tuhuma za kutoa huduma za afya ikiwemo matibabu na upasuaji bila kuwa na cheti cha taaluma ya udaktari.
Tukio hilo limethibitidhwa na Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma Giles Muroto, ambaye amesema, mtu huyo amekuwa akiendesha shughuli zake katika hospitali mbalimbali za wilaya ya Chemba mkoani humo.
''Huyu ndugu hana cheti na amekuwa akifanya upasuaji mdogo kwa wananchi wenye uvimbe na vidonda na amekiri wazi katika mahojiano kuwa amekuwa akifanya hivyo kupitia hospitali za watu binafsi'', amesema.
Aidha Muroto amebainisha kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na mahojiano zaidi na Bw. Hassan ili kujua kwanini anafanya kazi hiyo bila kuwa na taaluma jambo ambalo ni hatari kwa afya za watu.
Pia ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa jeshi la polisi juu ya watu wasio na mienendo mizuri kwenye jamii kwani vitendo hivyo havina nafasi ndani ya mkoa wa Dodoma.