Dar yaburuzwa na Dodoma Ukusanyaji Mapato

Katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2018/19, Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeongoza katika ukusanyaji mapato ya ndani, ikiendelea kuliacha mbali Jiji la Dar es salaam na baadhi ya majiji mengine ya mwanzo.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo alipokuwa akitoa ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa robo ya kwanza ya mwaka, ambapo amesema Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeongoza kwa kukusanya mapato ghafi ya Sh bilioni 14.49 kati ya makisiso ya kukusanya Sh bilioni 68.6 ambayo ni sawa na asilimia 21.

Aidha, Arusha inaongoza kwa kukusanya vizuri kiasilimia na imefanikiwa kukusanya Sh bilioni 4.1 kwa asilimia 26 ya malengo waliyojiwekea ya kukusanya Sh bilioni 15.6.

“Ieleweke wazi kuwa Jiji la Arusha ndio lililofanya vizuri kimakusanyo kwa mujibu wa asilimia lakini Jiji la Dodoma ndio lililokusanya fedha nyingi zaidi kuliko halmashauri zote Tanzania,” amesema.

Kwa mwaka wa fedha 2018/19, halmashauri zilipangiwa kukusanya Sh bilioni 735.6 kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani na hadi kufikia Septemba 30, mwaka huu, halmashauri zimekusanya jumla ya Sh bilioni 143.6 sawa na asilimia 20 ya makisio ya mwaka.

Jafo alisema mwaka wa fedha 2017/18, halmashuri zilipangiwa kukusanya Sh bilioni 687.3 na hadi Septemba 30, mwaka 2017, ziliweza kukusanya Sh bilioni 126.8 sawa asilimia 18 ya makisio ya mwaka.

"Kutokana na takwimu hizo, inaonyesha Halmashuri zimeongeza wingi wa mapato kwa Sh bilioni 16.7 na ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani umeongezeka kwa asilimia mbili, uchambuzi wa mapato ya ndani ya robo mwaka ya mwaka wa fedha 2018/2019, unaonesha kuwa halmashauri 76 zimefanya vizuri kwa kukusanya zaidi ya asilimia 20 ya makisio yake ya mwaka," ameongeza.

“Kati ya halmashauri hizo Majiji ni manne, zikiongozwa na Arusha, manispaa saba zikiongozwa na ya Musoma, miji 12 ikiongozwa na mji wa Mbinga na Wilaya 53 zikiongozwa na wilaya ya Kisarawe.”
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad