Didier Drogba Astaafu Rasmi Soka

Didier Drogba Astaafu Rasmi Soka
Mchezaji wa zamani wa Chelsea na timu ya taifa ya Ivory Coast Didier Drogba, amestaafu rasmi kucheza soka, baada ya kucheza mchezo wake wa mwisho katika fainali ya kombe la USL ambao klabu yake ya Phoenix Rising FC imepoteza usiku wa kuamkia leo.


Drogba, ambaye ni mwekezaji mwenza katika klabu ya Phoenix tangu mwaka 2017, alitangaza hapo awali kuwa atastaafu mwishoni mwa msimu huu, ambapo sasa muda wake rasmi umewadia baada ya kupoteza kwa 1-0 dhidi ya Louisville City FC.

Haijajulikana bado ni kitu gani ambacho mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 40 anapanga kufanya baada ya kustaafu rasmi soka, ingawa aliwahi kusema kuwa atageukia katika masuala ya kiuongozi ndani ya klabu hiyo.

"Mpango huo unafanyika vizuri, fursa hii ni ya kushangaza kwa sababu inaniweka moja kwa moja ndani ya kile nataka kujifunza. Nifurahia ukweli zaidi kwamba ninajifunza mengi kuhusu upande mwingine wa mchezo, ambao ni muhimu sana," alisema Drogba mwaka uliopita.

Mchezaji huyo bora wa mwaka wa Afrika mara mbili alianza safari yake ya soka nchini Ufaransa katika klabu ya Marseille .

Alifanikiwa kukaa kwa muda mrefu katika klabu ya Chelsea, ambapo alifunga mabao 157 katika michezo 341 aliyocheza klabuni hapo kwa misimu nane. Alirejea klabuni hapo msimu wa 2014-15 ambapo alishuhudia Chelsea ikishinda ubingwa wa ligi kuu nchini Uingereza EPL.

Baada ya kucheza soka kwa miaka mitatu nchini China na Uturuki, Drogba alielekea Amerika ya Kaskazini, katika klabu ya Montreal Impact msimu wa  2015/16, na kisha kujiunga na Phoenix Rising Fc baada ya kuwa mmoja ya wawekezaji katika klabu hiyo mwaka uliopita.

Alistaafu kucheza soka la kimataifa nchini Ivory Coast mwaka 2014 baada ya Kombe la Dunia nchini Brazil, akiwa amefunga mabao 63 katika mechi 104 kwa muda wa miaka 12 aliyoitumikia nchi yake.

Mataji aliyoshinda mpaka alipostaafu rasmi ni pamoja na Klabu Bingwa Ulaya, EPL (4), FA (4), Kombe la ligi (3), Ngao ya Jamii (2), Kombe la Uturuki, Turkish Super Cup, Mataifa ya Afrika (2) na mafanikio mengine mengi binafsi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad