Fatma Karume na Tundu Lissu waichambua hukumu ya Nondo



Dar es Salaam. Baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa kumwachia huru Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi (TSNP), Abdul Nondo, baadhi ya wanasheria wamelitaka Jeshi la Polisi litumie hukumu hiyo kuboresha utendaji wake.

Kwa mara ya kwanza, Nondo alifikishwa mahakamani hapo Machi 21 akikabiliwa na makosa mawili ya kuchapisha taarifa za uongo kwamba “nipo hatarini” na kuzisambaza mitandaoni pamoja na kutoa taarifa za uongo kwa polisi kuwa alitekwa, mashtaka ambayo yalitupiliwa mbali na mahakama.

Jana, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume alisema licha ya hukumu hiyo kugubikwa na wingu la kisiasa, uamuzi wa mahakama umerejesha imani kwa wananchi kuwa ni chombo huru huku akisisitiza kuwa iwe funzo kwa Jeshi la Polisi kuboresha utendaji wake.

“Nimesoma judgement (hukumu)ya mahakama ina busara, imefuata sheria na imeonyesha kuwa ni chombo huru na haijakubali kuingiliwa,” alisema Fatma.

Katika kesi hiyo, Hakimu Mfawidhi Liad Chamshana alisema upande wa Jamhuri ulishindwa kuthibitisha mashtaka mawili likiwamo kosa la mshtakiwa kuripoti kituo cha polisi cha Mafinga kabla ya malalamiko yake kugeuzwa kuwa mashtaka. Fatma alisema, “Kwa hiyo natumaini kwamba polisi wataitazama hiyo judgement vizuri na kutazama ni wapi wamekosea na ni wapi pa kujirekebisha,” alisema.

Kauli ya Fatma iliungwa mkono na mtangulizi wake, Tundu Lissu ambaye katika waraka wake alizungumzia kesi hiyo akisema imetoa somo kwa vyombo vya ulinzi na usalama kujitathmini upya.

“Hukumu ya Nondo inatupa fursa si tu ya kujua kilichomtokea yeye binafsi, bali pia kudai na kupatiwa majibu sahihi ya matukio mengine ya aina hii ambayo hayapewa majibu sahihi na ya kuridhisha,” aliandika Lissu.

Nondo alisema baada ya kusimamishwa masomo na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), utaratibu wa kurudi chuoni hapo unaendelea ikiwamo kuwasilisha barua pamoja na hukumu ya mahakama.

“Si sheria zote ambazo ni sahihi, kuna sheria ambazo ni kandamizi kwa hiyo ni chachu ya kuangalia namna gani sheria hizi zinaweza kubadilishwa. Tunapokuwa na sheria kwenye taasisi zetu ambazo zinamhukumu mtu kabla ya mahakama si jambo sahihi,” alisema Nondo.

By Cledo Michael, Mwananchi cmichael@mwananchi.co.tz
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad