KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Haruna Niyonzima, mambo yake ni magumu ndani ya klabu hiyo na taarifa zinaeleza anataka kusepa baada ya kukosa nafasi katika kikosi cha kwanza.
Tangu atue kuichezea klabu hiyo Agosti, mwaka jana, Niyonzima ameanza mechi tisa tu Simba, lakini ameshavuna zaidi ya Sh milioni 232, fedha ambayo ni nyingi sana ukilinganisha na mchango anaotoa.
Ukijumlisha fedha ambazo ameshaingiza hadi sasa Simba, ambazo ni Sh milioni 232 ukigawa mechi tisa alizoanza, utabaini kuwa kimahesabu Simba inamlipa Sh 25,777,777 katika kila mechi anayoanza.
Tangu wakati huo, Niyonzima pia ameifungia Simba bao moja tu ligi kuu. Kama ukiliweka katika mahesabu ya kiuchumi, utabaini kuwa bao hilo linagharimu Sh milioni 232.
Tangu ajiunge na Simba msimu uliopita akitokea Yanga, Niyonzima ameshindwa kuonyesha cheche zake alizokuwa akizionyesha Jangwani.
Amekuwa hapati nafasi. Niyonzima ndiye mchezaji pekee wa kimataifa wa Simba kati ya wale waliosajiliwa msimu uliopita ambaye ameitumikia timu hiyo mechi chache zaidi za ligi kuu kuliko wengine.
Tangu Niyonzima ajiunge na Simba, mpaka sasa inaelezwa kuwa ameshajikusanyia zaidi ya Sh milioni 232.
Fedha hizo ni pamoja na Sh milioni 115 za usajili, Sh milioni 112 za mshahara ambazo amelipwa kwa kipindi cha miezi 14 ambayo amekuwa na timu hiyo tangu Agosti, mwaka jana. Lakini pia amelipwa zaidi ya Sh milioni 5,120,000.
Alipoulizwa Niyonzima kuhusiana na hilo alisema anajifua ili arejeshe ubora wake. Lakini Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Patrick Aussems, alisema: “Katika kikosi changu mchezaji anayepata nafasi ya kucheza ni yule anayefanya vizuri mazoezini, Niyonzima kwa muda mrefu hakuwepo kikosini.”
MWANDISHI WETU, Dar es Salaam