Hatimaye kocha wa taifa Stars afanya maamuzi kwa Kichuya


Hatimaye kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike amemuita kiungo Shiza Ramadhani Kichuya katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania kwa ajili ya mchezo dhidi ya Lesotho katikati ya mwezi huu kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon. 

Taifa Stars watakuwa wageni wa Mamba wa Lesotho Novemba 18, mwaka huu Uwanja wa Setsoto mjini Maseru katika mchezo wa Kundi L kufuzu AFCON ya mwakani na Amunike baada ya kumpuuza katika mechi tatu zilizopita Kichuya, sasa amempa nafasi. 

Winga wa zamani wa Barcelona na Nigeria, Amunike ameimarisha safu yake ya kiungo kwa kumchukua Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kuziba pengo la kiungo mwenzake wa Azam FC, Frank Domayo ambaye majeruhi pia. 

Kwa kiasi kikubwa Amunike amerejesha kikosi kilichompa ushindi wa 2-0 dhidi ya Cape Verde Oktoba 16 mjini Dar es Salaam kikitoka kuchapwa 3-0 mjini Praia na Papa wa Bluu Oktoba 12. 

Kikosi hicho chini ya makocha Amunike anayesaidiwa na Mnigeria mwenzake, Emeka Amadi na mzawa Hemed Suleiman ‘Morocco’, Meneja Danny Msangi, Mtunza Vifaa Ally Ruvu na Madaktari Richard Yomba na Gilbert Kigadya kitaingia kambini nchini Afrika Kusini wiki ijayo kabla ya kwenda Lesotho siku moja kabla ya mchezo wa Novemba 18. 

Baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Cape Verde Oktoba 16 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Taifa Stars sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi L kuwania tiketi ya Cameroon mwakani, ikifikisha pointi tano baada ya kucheza mechi nne, ikifungwa moja na sare mbili. 

Uganda ambayo siku hiyo iliifunga tena Lesotho 2-0 mjini Maseru, ndiyo inaongoza kundi hilo kwa pointi zake 10 za mechi nne, wakati Cape Verde inabaki na pointi zake nne katika nafasi ya tatu. Lesotho ndiyo inashika mkia kwa pointi zake mbili. 

Taifa Stars itahitimisha mechi zake za Kundi L kwa kumenyana na Uganda Machi 22 mwakani, miezi miwili tu kabla ya kuanza kwa AFCON ya mwakani.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad