Hii Ndiyo Faida Ya Kupanda Mbegu Bora Kwa Wasaidizi Wako Wa Kazi Katika Familia Yako.
0
November 10, 2018
Kumekuwa na matukio mbalimbali yanatokea yakihusu wafanyakazi au wasaidizi wa kazi za ndani. Matatizo mengi yanatokea katika familia nyingi hayaji tu kama radi lazima kuna sababu zinazopelekea kutokea kwa matatizo hayo. Huwezi kupanda mahindi shambani halafu ukategemea kuvuna mbaazi.
Hivyo siku zote utavuna kile ulichopanda. Kama ukipanda mbegu bora ya upendo katika familia yako tegemea kuvuna mbegu bora ya upendo. Vivyo hivyo, kama ukipanda chuki katika familia yako tegemea kuvuna mauti. Hii ni sheria ya asili unapokea kile unachotoa.
Kwa tafiti zisizo rasmi, ukitembelea nyumba kumi kati ya nyumba hizo kumi moja tu ndio wanaishi vema na wasaidizi wao wa kazi za ndani. Nyumba nyingi ni matatizo sana je matatizo haya yote yanasababishwa na nani? Lazima tuchunguze nini kiini cha kosa au tatizo kwanza. Huwezi kutatua tatizo bila kuchunguza kiini cha kosa.
Visa vimekuwa vikitawala ndani ya nyumba nyingi kwa wale wanaoishi na wasaidizi wao wa kazi za ndani. Wasaidizi wa kazi za ndani wanafanyiwa ukatili na waliowaajiri ndio maana nao wanalipa visasi kwa watoto wao. Wasaidizi wa kazi za ndani wanarusha visasi wanavyofanyiwa na waajiri wao kwa watoto.
Watoto wanakua wahanga wa matatizo mengi wanaumizwa na kuteswa na kuona dunia ni chungu na siyo sehemu salama ya kuishi kutokana tu na kuishi maisha yaliyokosa upendo ndani yake. Waajiri wa kazi za ndani wanapandikiza chuki kwa wafanyakazi wao wa ndani na wasaidizi wao wanaona sehemu sahihi ya kulipiza kisasi ni kwa watoto.
Hivyo wasaidizi wa kazi za ndani nao wanatoa kile walichopokea na siku zote chuki huzaa mauti. Ndio maana kuna faida kubwa sana kwa waajiri kupanda mbegu ya upendo ambayo itakwenda kuota kwa kila mwanafamilia na hatimaye watakuja kuvuna upendo.
Mpendwa msomaji, jaribu kuvuta picha ni matukio mangapi umeyasikia au kuyaona kwa macho yako yanayosababishwa na wafanyakazi wa ndani. Na je wahanga wakubwa wa matatizo hayo katika familia ni kina nani? Kama sio watoto? Wafanyakazi wa ndani ndio wanaonekana wana makosa au wakosa kama hujachunguza kiini cha tatizo au kosa kwanza.
Wanawake wengi walio na waume zao wanawaachia wadada wa ndani kila kitu wafanye hata zile kazi ambazo hawapaswi kufanya, kazi ambazo angetakiwa kufanya na mama au mwanamke aliyeolewa ambaye yeye ndio mlinzi wa familia. Wanawake wengi wanawatengenezea mazingira mabaya wao wenyewe na unakuta nafasi ya mke sasa anachukua dada wa kazi. Kwa kisingizio kua yuko bize na kazi mpaka anasahau wajibu wake kama mke au mama wa familia.
Lazima muwe na mipaka ya kazi na wasaidizi wenu wa kazi siyo kumuachia akufanyie kila kitu katika nyumba yako unayoishi. Wasaidizi wa kazi za ndani unakuta wanajua vitu vingi kuliko mama wa familia ndani ya nyumba sasa hii ni hatari sana.
Kutokana na mwanamke katika familia yake kushindwa kuwa mlinzi wa familia yake matokeo yake hata wale wanaume wasiokua waaminifu katika ndoa zao wanatembea na wasaidizi wao wa kazi kwa sababu mazingira hayo wanayasababisha wao wenyewe. Unampatia msaidizi wako wa kazi kufua nguo za muwe wako hata za ndani na kumwandalia kila kitu mume wako unafikiri unategemea nini?
Hujaolewa kwenda kuwa mtalii wa nyumba bali mwanamke aliyeolewa anakwenda kuwa mlinzi wa nyumba yake na baba kuwa kichwa cha familia yake. Na kazi hizo wamepewa na Mungu. Ndio jukumu la mke na mume wakishindwa kutimiza wajibu wao kila mmoja kinachofuata ni machozi tu.
Ukiwa ni mama wa kutoa agizo dada naomba nenda kamtandikie baba anataka kulala, au kamuandalie maji ya kuoga, chakula, mwangalie mtoto kama amekula, kama anaumwa, waangalie watoto kama wameenda shule nk na wewe umekaa sebuleni unaangalia tv na kubadilisha chaneli utakuja kupata hasara tu.
Kama wewe ni mwanamke ndani ya nyumba usikwepe majukumu yako na kumwachia dada wa kazi na wewe kama ni baba wa familia simama kama kiongozi kweli na mwanamke linda nyumba yako.
Mpendwa msomaji, unajua ni kwa nini matatizo yanatokea kwa wasaidizi wa kazi za ndani?
Sasa karibu ujionee viini vya matatizo hayo.
1. Kukosa upendo;
wasaidizi wa ndani wanakosa upendo badala yake wanapewa chuki ambayo ndio inakuja kuzaa matatizo mengi katika nyumba nyingi. Hakuna kitu kama upendo wewe lisikie tu neno hili upendo lina maana kubwa sana kwa binadamu.
Kama vile wewe unahitaji kupewa upendo na watu wengine mpatie na msaidizi wako wa kazi naye anakurudishia upendo. Mpende kama unavyojipenda wewe, kama unavyoipenda familia yako na mfanye awe sehemu ya familia yako. Vaa viatu vyake halafu utaona kama utavuna ubaya kutoka kwake.
2. Kukosa kuthaminiwa;
mwanasaikolojia mmoja aliwahi kusema, hitaji la kwanza la binadamu ni kuthaminiwa. Anza leo kumthamini mfanyakazi wako uone naye atakavyokuwa anakuthamini. Unatoa kile unachopokea katika maisha yako.
Binadamu akihisi anakosa kuthaminiwa anakua amekufa kisaikolojia kabisa. Ni nani ambaye hahitaji kuthaminiwa? Kila mtu anataka kuthaminiwa katika hii dunia. Hakuna mtu aliyezaliwa kuja kupata mateso duniani mwache kila mtu afurahie na kuonja thamani yake hapa duniani.
3. Kukosa uhuru;
kukosa uhuru ni utumwa katika maisha. Ndio maana watu wanapelekwa gerezani kufungwa ili wakose ule uhuru wao. Kila mtu anahitaji uhuru. Sasa hawa wasaidizi wa ndani hawapewi fursa ya uhuru. Ukimbana sana mtu na kukosa uhuru na ni mtu mzima lazima atatafuta uhuru. Naye ni binadamu anahitaji uhuru kama wewe, uhuru wa kufanya mambo yake na usimtawale kama vile mtoto mdogo.
4. Kudharauliwa, kutengwa na kuchukuliwa kama siyo sehemu ya familia;
wasaidizi wa ndani wanachukuliwa kama watu wenye shida sana, siyo wa umuhimu na hafai kuwa sehemu ya familia. Wanalala sehemu isiyostahili kulala, wanavaa mavazi yasiyo nadhifu yaani ukienda nyumba nyingine unatamani hata kutokwa na machozi watoto wa familia wamevaa nguo nadhifu ukimuona yeye kachoka kabisa anachukuliwa siyo mtu muhimu.
Mtu anayekupikia, kukuangalizia watoto na nyumba yako halafu unamdharau ndio maana hata wengine wanawekewa sumu kwa sababu ya mateso wanayofanyiwa na wanafamilia. Wakati wa kula chakula dada wa kazi anakula jikoni peke yake wanafamilia wamekaa mezani wanakula hivi wewe ungekuwa unafanyiwa hivi ungejisikiaje? Wakati mwingine hata chakula wanapewa masalia wanafamilia kwanza. Ishi na msaidizi wako kwa upendo.
5. Kutukanwa, kupigwa na kudharauliwa;
baadhi ya wasaidizi wengine wanateswa na wanatukanwa matusi ya kila aina yaani wamegeuzwa kama jalala la matusi. Mwisho wa siku dada wa kazi anakua anapata majeraha ya moyo. Wengine wanapigwa na kuteswa na kunyimwa hata chakula. Halafu ukifanyiwa jambo baya utasikia wafanyakazi wa ndani sio watu siku hizi.
Kabla ya kulalamika chunguza kiini cha kosa ni nani msababishi wa yote haya? Wanafamilia wanatendea vibaya wadada wa kazi ndio maana nao wanawatendea mabaya. Ndio maana dawa ya chuki huzaa mauti, unamfanyia mwenzako mabaya halafu unategemea mazuri? Sahau kuhusu hilo.
6. Kusemwa maneno makali;
wanasemwa maneno makali yenye chuki ambayo yanakwenda kutengeneza majeraha katika moyo. Maneno ni mabaya kwani yanakwenda kutengeneza chuki ndani ya moyo. Acha kuwasema sana maneno mabaya bali mtie moyo na hamasa ya kufanya kazi na kushirikiana naye hata kama unamlipa. Kuwa kiongozi mzuri katika familia yako.
7. Kutopewa nafasi ya kujieleza na kushindwa kumpata mtu wa kumuelezea matatizo yake; nguvu ya pesa wakati mwingine huwa inatumika kwa kuwakandamiza wadada wa ndani. Ananyimwa mahitaji ya msingi anaingiwa na tamaa ya kuiba halafu akiiba nguvu ya pesa inatumika anakamatwa na kupelekwa polisi bila hata kupewa nafasi ya kujieleza.
Na kukichunguza kiini cha kosa utagundua mwajiri wake ndiye msababishi. Unakuta wakati ana shida anakosa mtu wa kumwambia watu wote ndani ya familia wamegeuka kuwa miiba hivyo anaendelea kubaki na uchungu ulioumbika na matokeo yake wanafanya matukio ya ajabu.
8. Kupewa ujira mdogo na kucheleweshewa ujira wao; dhahiri kwamba wafanyakazi wengi wa ndani wanalipa ujira mdogo na wanafanya kazi nyingi zaidi ya masaa 12 bila mapumziko. Kama anakufanyia kazi zako mpe stahiki yake hata kama ni kidogo.
Kama humpatii mahitaji yake binafsi lazima umpatie hela ili aweze kujitegemea. Kuna wengine hawapewi kabisa wanaambulia maneno kama haya unakula bure tu, kulala hapa na kujaza choo hapa. Mambo kama haya unakuwa unamuumiza msaidizi wako.
Mwisho, ndugu msomaji, panda mbegu bora ya upendo kwa manufaa yako na kwa jamii nzima. Mpe malazi mazuri na chakula bora. Mtendee mwenzako kama vile unavyotaka wewe kutendewa na vaa viatu vya mwenzako. Kuwa mfano sahihi kama unamwambia msaidizi wa kazi kuamka saa 11 au 12 na wewe onesha mfano. Siyo wewe unatoa agizo halafu unaamka saa 2 jihukumu kwanza wewe mwenyewe kabla ya kumhukumu mwenzako.
Tags