Mtangazaji maarufu wa kituo cha Star TV na Radio Free Africa, Samadu Hassan amefariki dunia usiku wa kuamkia leo nyumbani kwake eneo la Miembe Mitatu Mkuyuni jijini Mwanza.
Akizungumza na www.eatv.tv, mtu wa karibu wa marehemu Samadu, amesema marehemu alikuwa akisumbuliwa na kifua kwa zaidi ya wiki moja, kabla ya kufikwa na umauti usiku ambapo alizidiwa ghafla.
“Samadu jana alikuwa kazini lakini kwa mujibu wa familia yake jana usiku alikuwa akilalamika kuwa kifua kinamsumbua na akaomba apumzike angekwenda hospitali kesho asubuhi ambayo ni leo", amesema.
Amesema kuwa ilipofika saa sita kasoro usiku, ghafla hali yake ilianza kubadilika na alianguka chini na kuanza kutokwa na mapovu mdomoni ndipo walipomkimbiza hospitali.
Marehemu Samadu mwili wake umehifadhiwa katika hospitali ya mkoa wa Mwanza Sekou Toure, ambapo mwili wake utasafirishwa kesho kupelekwa nyumbani kwao mkoani Kagera kwaajili ya maziko.