Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan amewasili Mererani wilayani Simanyiro mkoani Manyara kwa ziara ya siku 5.
Makamu wa Rais amepokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti, Wabunge pamoja Viongozi wa Serikali na Chama cha Mapinduzi ambapo alipokea taarifa ya mkoa iliyosomwa na Mkuu wa Mkoa.
Pamoja na mambo mengine Mkuu wa Mkoa wa Manyara alimueleza kuongezeka kwa mapato katika mkoa huo sambamba kuongezeka kwa makusanyo mara baada ya kujengwa kwa ukuta.
“Miezi 10 kabla ya kujengwa kwa ukuta tulikuwa tunakusanya milioni 402 na miezi 10 baada ya ukuta tunakusanya bilioni 2.1,” alisisitiza Mkuu wa Mkoa.
Makamu wa Rais ameushukuru uongozi wa mkoa kwa mapokezi mazuri na kuupongeza kwa hatua mbali mbali za kimaendeleo pamoja na kuboresha huduma za jamii ikiwemo huduma maalum kwa wazee.