Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo amefunguka baada ya timu ya taifa ya Tanzania, taifa stars kufungwa goli 1-0 dhidi ya Lesotho katika mchezo wa kufuzu michuano ya AFCON.
Baada ya mchezo huo taharuki iliibuka katika mitandao ya kijamii, huku wengi wao wakielekeza lawama kwa Kocha wa timu hiyo, Emmanuel Amunike kutokana na namna walivyopanga kikosi cha kwanza.
Jokate kupitia ukurasa wake wa 'twitter' ameandika kuwa baada ya kutua nchini timu hiyo inatakiwa ikafanye kazi ya kubangua korosho zilizonunuliwa na serikali, ikiwa ni adhabu ya kile walichokifanya.
"Kubangua korosho kunawahusu aisee", ameandika Jokate.
Pia kufuatia matokeo hayo, kiongozi wa chama cha ACT-wazalendo ambaye ni shabiki mkubwa wa Taifa Stars ametoa maoni yake kwa timu hiyo katika mtandao wa Twitter kwa kuandika,
"Ukweli ni Kwamba tulijiandaa kushangilia. Hatukujiandaa kushinda, bado tuna nafasi kwenda #AFCON2019, #TaifaStars Muhimu tujiandae kucheza mechi yetu na mechi ya Lesotho v Cape Verde ili kupata matokeo. Tunao muda, Amunike tumshukuru, aende. Tumtafute Kim Paulsen."
Taifa Stars inahitaji kupata matokeo ya ushindi katika mchezo wake wa mwisho dhidi ya Uganda huku ikiiombea Cape Verde ipate ushindi dhidi ya Lesotho ili iweze kufuzu kwa tofauti ya alama moja. Matokeo tofauti na hayo, Taifa Stars itakosa nafasi ya kufuzu michuano hiyo.