Kesi inayomkabili, aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na wenzake wanne imekwama kusikilizwa kwa sababu kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Richard Rweyongeza anaumwa.
Kesi hiyo imekwama kuendelea leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.
Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai amedai kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kusikilizwa, wamejiandaa na shahidi yupo mahakamani.
Wakili wa utetezi, Abraham Senguji aliieleza mahakama kuwa kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Wakili Rweyongeza bado anaumwa.
Wakili Rweyongeza yeye ndiye aliyemsikiliza shahidi wa nane anayeendelea kutoa ushahidi katika kesi hiyo upande wa mashtaka kwa kirefu, aliomba wapewe ahirisho fupi ili aweze kuwepo.
Hakimu Mashauri baada ya kusikiliza pande hizo mbili aliiahirisha kesi hiyo hadi Novemba 15, 2018 kwa ajili ya kutajwa.
Mahakama ilipanga Novemba 21 na 22, mwaka huu kesi hiyo itasikilizwa kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.
Shahidi huyo wa nane wa upande wa mashtaka ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Kidao Mzigama Wilfred (41).
Washtakiwa katika kesi hiyo mbali na aliyekuwa rais TFF, Jamal Emil Malinzi(57) wengine ni Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Joas Selestine(46) na Mhasibu wa TFF, Nsiande Isawayo Mwanga(27).
Meneja wa Ofisi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Miriam Zayumba na Karani wa TFF, Flora Rauya ambao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 30 katika kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha wa Dola za Marekani 173,335 na Sh 43,100,000.
Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wapo rumande kwa kukabiliwa na mashtaka ya utakatishaji wa fedha kuwa miongoni mwa mashtaka ambayo kwa mujibu wa sheria hayana dhamana huku wenzao Zayumba na Frola wapo nje kwa dhamana.