Kibano zaidi Malipo Posho kwa Watumishi wa umma


MSAJILI wa Hazina, Athumani Mbuttuka, ameshtukia malipo ya posho mbalimbali kufanyika kinyume cha utaratibu na kutaka jambo hilo kusimamishwa mara moja.


Ameagiza kuwa matumizi yote ya fedha za serikali hasa malipo ya posho, marupurupu na maslahi mbalimbali ya bodi, viongozi wa taasisi na watumishi  kufanyika kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya serikali.

Mbuttuka alitoa agizo hilo jana alipokuwa akifungua semina kwa watendaji wakuu, wenyeviti na wajumbe wa bodi kuhusu usimamizi wa taasisi na mashirika ya umma.

Alisema matumizi mengi katika taasisi za umma yamekuwa hayazingatii sheria, kanuni na miongozo hali ambayo imekuwa ikisababisha uwapo wa matumizi mabaya ya fedha za umma.

Aidha, alizitaka taasisi za umma kujiwekea mikakati ya kupunguza gharama za uendeshaji zitokanazo na matumizi yasiyo ya lazima hususan safari za bodi na viongozi zisizo na tija kwa ofisi.

"Malipo ya posho za nyumba, simu na umeme yanapaswa kufanyika kwa watumishi wenye stahili hizo tofauti na utaratibu uliojengeka kwa watumishi kulipwa posho hizo," alifafanua Mbuttuka.

Msajili alizitaka Bodi za Wakurugenzi za taasisi zote za umma kuhakikisha vikao vyake vinafanyika kwa mujibu wa sheria na taratibu husika.

"Mnatakiwa kuhakikisha kuwa nyaraka mbalimbali zinazotumiwa hususani miundo ya utumishi, kanuni za utumishi, kanuni za fedha, mfumo wa motisha zinapitishwa na mamlaka na kupata idhini kabla ya kutumika," alisema.

Pia aliagiza kuwa nyaraka zote zinazotumika sasa pasipo idhini ya Msajili wa Hazina na Katibu Mkuu Utumishi ziwasilishwe ofisini kwake kwa ajili ya kupatiwa idhini.

Aidha, alizitaka taasisi zote zinazopaswa kuchangia asilimia 15 ya mapato ghafi katika mfuko mkuu wa serikali, kuhakikisha zinatekeleza wajibu huo kwa mujibu wa sheria.

"Zaidi ya kuwasilisha malipo hayo kila robo ya mwaka, bodi inatakiwa kuhakikisha mchango unaowasilishwa uko sahihi, halisi na unaendana na kiwango cha malipo ghafi ya taasisi au shirika, tofauti na hali ilivyo sasa inayomlazimisha msajili wa hazina kufuatilia, hivyo kuongeza gharama za ufuatiliaji kwa serikali," alisema.

Sambamba na hilo, alizitaka bodi zote kuhakikisha zinazingatia mikataba ya utendaji kazi na msajili wa hazina kwa mujibu wa sheria ya msajili wa hazina kifungu cha 10 (2) (k).

Alisema taasisi zote zenye utendaji usioridhisha na zile zinazopata hasara kila mwaka wanatakiwa kuwa wabunifu na kuweka mikakati ya kuboresha utendaji wao.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad