Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, ametoa siku nne kwa vyama vya ushirika vilivyopo mkoani humu kuhakikisha wanaziondoa korosho katika maghala yao na kuzipeleka katika maghala makuu matatu yaliyoelekezwa na Serikali likiwamo la Kibiti, Mkuranga na Tanita kabla hazijaanza kununuliwa wiki ijayo.
Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana alipozungumza na viongozi wa idara za mkoa na wilaya baada ya kutembelea ghala la kuhifadhi korosho na kiwanda cha kubangulia zao hilo kilichopo eneo la Tanita, Halmashauri ya Mji wa Kibaha.
Alisema hatua hiyo ni mchakato wa Serikali kuanza kununua korosho kwa njia rahisi na salama ili kuhakikisha wakulima wanapata stahiki yao kama ambavyo Rais Dk. John Magufuli ameagiza.
Alisema Pwani ina vyama vya ushirika zaidi ya 80 na hadi sasa wamehifadhi korosho hizo katika maghala yao hivyo huu ni wakati mwafaka wa kuhakikisha zinahamishiwa katika maghala makuu ya Serikali ili ununuzi ufanyike mara moja.
“Wenzetu Mtwara, Lindi na Ruvuma tayari wanaendelea kuuza korosho kama ambavyo mnasikia, lakini kwa upande wa Pwani tunaanza kununua korosho wiki ijayo kwa hiyo ili kuleta urahisi lazima korosho hizo zipelekwe katika maghala makuu matatu yaliyopangwa na Serikali,” alisema.
Ndikilo alisema Ghala la Tanita lina uwezo wa kuhifadhi tani 2,000, Kibiti tani 5,500 na Mkuranga tani 10,000.
Alisema baada ya korosho hizo kukusanywa katika maghala hayo, wataalamu watazipima kulingana na mwongozo wa Serikali na kisha mkulima kulipwa fedha zake bila usumbufu na baadaye magari ya jeshi yatakuja kuzisomba kama inavyofanyika Mtwara.
Alivitaka vyama hivyo kuendesha mchakato huo kwa haraka ili kuhakikisha wakulima wanafaidika kwa kuuza korosho zao kwa wakati kwa kuwa kuchelewesha kutachelewesha wakulima kulipwa