Lugola Asema Ili Upate Kitambulisho Cha Taifa Lazima Upitie Katika Mchujo Mkali


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema vitambulisho vya taifa vitatolewa kwa watanzania wenye sifa ambao watapita katika mchujo ili kuepusha kutoa kwa wahamiaji haramu.

Amesema mchujo huo unaofanywa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) upo makini ili kuhakikisha hakuna makosa yatakayofanywa wakati wa utoaji wa vitambulisho, hivyo wananchi wawe na uvumilivu wakati mchujo huo ukiendelea.

Waziri Lugola ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mwibara aliyasema hayo jana, wakati alipokua anazungumza na mamia ya wananchi wa jimbo lake katika Kijiji cha Mwisenyi, Kata ya Butimba, Wilayani Bunda Mkoa wa Mara na kuwataka wapiga kura wake na Watanzania kwa ujumla wawe na subira wakati hatua za utambuzi na usajili zikiendelea kufanyika sehemu mbalimbali nchini.

“Hakuna Mtanzania mwenye sifa atakayekosa kitambulisho cha taifa, lakini lazima muwe na subira wakati zoezi la utambuzi wa watu gani wanaweza kupata vitambulisho hivi, na pia katika utambuzi tunapaswa kuwa makini sana kwasababu tusije tukapenyeza wahamiaji haramu wasiostahili na wao wakaweza kupata vitambulisho na baadaye tukaja kupata shida,” alisema Lugola.

Lugola alisema baada ya hatua ya utambuzi, inafuata hatua ya usajili ambayo pia hatua hiyo nayo inahitaji umakini mkubwa zaidi na ikimalizika hatua hiyo majina yaliyosajiliwa yanarudishwa tena kwa wananchi kuulizwa kama waliosajiliwa wanatambuliwa katika sehemu wanazoishi, hatua hiyo ikiwa na lengo la kupata taarifa sahihi ya waliosajiliwa wanatambuliwa au hawatambuliwi na wazawa katika eneo husika.

“Endapo majina tulioyasajili na kuyaleta kwenu, nanyi mtayakataa basi hatutaweza kutoa vitambulisho kwa huyo au hao mliowakataa, na endapo mtayaridhia majina tuliyowaletea, basi tutaweza kuwatengenezea vitambulisho bila shaka yoyote, na endapo kuna mwananchi amekataliwa na Kijiji kuwa hatambuliwi, anayohaki ya kukata rufaa na kutueleza kwanini apewe kitambulisho,” alisema Lugola.

Lugola ambaye alikua anaulizwa maswali mbalimbali na wananchi hao kuhusu Nida na idara zake nyingine zilizopo ndani ya Wizara yake, aliwahakikishia wapiga kura wake kuwa, hakuna Mtanzania atakayekosa kitambulisho cha taifa, kila mwananchi ana haki ya kupewa akiwa ana sifa ya kupewa.

Aidha, Waziri Lugola aliwataka wananchi wa jimbo lake waanze maandalizi ya kilimo cha mazao ya chakula na biashara ili kuepuka janga la njaa lisije liwakumba endapo hawata lima. Hata hivyo, kijiji hicho alichokitembelea, kwa mujibu wa taarifa ya mipango yao ya kilimo walisema kuwa wana upungufu mkubwa wa mbegu za mazao mbalimbali hasa zao la pamba.

“Nimeagiza maafisa ugani waje kuangalia upungufu wa mbegu za pamba na kutatua kero hii kutokana na taarifa yenu ya mpango wa kilimo ya mwaka 2018/2019, na pia nasisitiza zaidi mulime mazao ya chakula kwa wingi,” alisema Lugola.

Pia Waziri Lugola alitoa shilingi milioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ya Kijiji hicho ambao ulisimama kwa zaidi ya miaka sita kutokana na ukosefu wa fedha, na pia aliendesha harambee kwa madiwani na maafisa alioambatana nao katika mkutano huo, na kufanikiwa kuchangisha shilingi milioni moja na elfu ishirini.

Lugola ameanza ziara jimboni kwake akisikiliza kero za wananchi pamoja na kuhamasisha kilimo cha mazao ya pamba, mahindi, mpunga, viazi na mengineyo ambayo wakazi wa jimbo lake wanalima mazao hayo kwa wingi.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Ninja...!!! Mie nasema na wale walioingia Kinyemela halafu wakala smaku humu humu ndani... kisha wakasomeshewa watoto zao... Halafu wakaingia katika Siasa baada ya kupigwa tafu na labda spika marehemu halafu akaanzisha chama cha mtu mmoja ambacha kiukweli hakina sifa za kuwa chama... Sasa huyu kweli atapita mchujo na aendelee kuhatarisha Amani yetu na utulivu au kutamrudisha kambini na kisha kuludi Makwao.... Lugola Tunakuamini katika Dhamana tuliyokupa utusafishie wavamizi na wahamiaji Haramu.....!!!

    Hapa kazi tu .. Tanzania ni Salama na

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad