Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad amesema mkataba wa utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi ulioitwa wa kihistoria na kutiwa saini Oktoba 23 mwaka huu ni batili.
Mkataba huo ambao ulihusisha Kampuni ya Utafutaji na Uchimbaji Mafuta ya Rak Gas kutoka katika nchi ya Ras Alkhaimah ya taifa la Umoja wa Falme za Kiarabu [United Arab Emirates-UAE] na Zanzibar ambao katibu Mkuu huyo amesema ni batili .
Amesema mkataba uliotiwa saini ni kwa ajili ya kugawana faida itayopatikana pindi uchimbaji wa mafuta au gesi utafanyika katika kitalu cha Zanzibar-Pemba [Production Sharing Agreement- PSA].
Maalim Seif akitoa sababu mbalimbali ikiwamo ya Muungano huku akiwataka Wazanzibar kuacha uvyama kuwa makini na suala hilo ambalo kwa namna moja ama nyingine alisema litakuja kuleta sintofahamu hapo baadaye.
“Hapa tuache uchama tuwe kitu kimoja si CUF Chadema wala CCM lazima hili suala la mafuta na gesi liangaliwe kwa kuwa lina kasoro nyingi ikiwemo kutokuwa na uwazi,”
“Suala la rasilimali ya mafuta na gesi lina umuhimu wa aina ya pekee kwa Zanzibar na watu wake kutokana na mazingira ya kikatiba, kisheria na kiuchumi hivyo basi bila ya kuwepo umakini, ukweli wa dhati wa wanaolisimamia na uwazi, Zanzibar, watu wake na vizazi vyao vya baadae watajikuta wameingizwa katika mgogoro mwengine mkubwa sana sawa au zaidi ya ule mgogoro wa mkataba wa Muungano,” amesema Maalim Seif.
Aidha, amesema kitendo hicho ni cha aibu na fedheha kwa Wazanzibar na wala wasitarajie kunufaika kama ambavyo Dk. Ali Mohamed Shein ametanabaisha kwa mujibu wa Maalim Seif huku akigoma bado kumtambua kama kafanya hivyo yeye ni rais.