Wiki iliyopita kulikuwa na matukio makubwa matatu ya burudani hapa Tanzania, na matukio yote matatu yalipangwa kufanyika siku ya Jumamosi Novemba 24, 2018.
Matukio mawili yalikuwa ni matamasha ya Tigo Fiesta na Wasafi Festival 2018 huku moja ikiwa ni show ya kawaida sio tamasha, ambayo iliandaliwa na msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Alikiba.
Show ya Alikiba ambayo ilifanyika Kahama katika uwanja wa Kambarage, ilipokelewa vizuri sana na mashabiki na kwa kifupi alisepa na kijiji kama ilivyokuwa kawaida.
Kwa upande wa Wasafi Festival, hao show yao ilienda sawa kwani shughuli za ufunguzi wa tamasha hilo zilifana na kwa ufupi walifanikiwa kukata kiu ya burudani kwa wakazi wa Mtwara.
Kwa wakazi wa Dar ambapo fainali ya tamasha la Tigo Fiesta ilipangwa kufanyika, kwa bahati mbaya sana tamashya hilo halikufanyika jambo ambalo lilizua taharuki kwa wadau na wapenzi wa burudani.
Watu wengi walishtushwa na taarifa za kusitishwa tamasha hilo, kwani taarifa ilikuja kutangazwa yakiwa yamebaki masaa machache kuanza kwa tamasha hilo.
Kusema ukweli haikuwa taarifa nzuri kwani kuna watu tayari walikuwa wamesafiri kutoka mikoani, na kuna wafanyabiashara wadogo wadogo ambao nao walijipanga kwa ajili ya kuuza bidhaa.
Ukiachaa na hasara walizopata wafanyabiashara hao wadogo wadogo. Hasara nyingine pia ni kwa wasanii ambao hao ndio tunaweza kusema wahanga wa matamasha kwa sasa ndio sehemu ambayo wasanii wanaitumia kujiingizia kipato.
Kwa sasa sio muda wa kuanza kulaumu ni nani mwenye makosa, juu ya kusitishwa tamasha hilo kwani pande zote mbili zilichelewa kuutangazia umma mapema.
Kama ni maombi ya kibali cha tamasha hilo kukataliwa, basi mamlaka husika wangetoa zuio hilo mapema pengine kabla ya siku tatu ya tukio.
Waandaaji nao wa Fiesta hawakutakiwa kuutangazia umma mapema kuwa Tamasha hilo lingefanyika Leaders ile hali hawakujua maombi yao kama yangekubaliwa au kukataliwa.
Hayo yametokea, kwa sasa ni muda wa waandaaji wa matamasha mengine makubwa ya muziki kama WASAFI FESTIVAL kutafakari zaidi maeneno mengine, na sio Leaders tena kwani eneo hilo lina masharti magumu kwa sasa hivi.
Hakuna sababu ya kung’ang’ania Leaders ile hali kuna maeneo mengi makubwa ya kufanyia matamasha hayo. Tumeona EFM matamasha yao ya MUZIKI MNENE na lile la KOMAA CONCERT yote hawajawahi kufanyia viwanja vya Leaders.
Huo ni ushahidi tosha kuwa sio lazima matamasha makubwa yafanyike Leaders, ingawaje hakuna ubishi viwanja vya Leaders vipo eneo zuri zaidi kibiashara. tofauti na viwanja kama Tanganyika Packers lakini lakini hakuna namna.
Huu ni muda muafaka kwa waandaaji wa matamasha makubwa ya kama Fiesta kufikiria nje ya Box pengine hata kukodi viwanja vya mpira, kwani tumekuwa tukiona mikoani na hata nchi jirani matamasha yakifanyika kwenye viwanja vya mipira why not Dar Es Salaam?.
Kwa ukubwa na wingi wa wasanii waliotakiwa kutumbuiza Tigo Fiesta Dar, bila shaka uwanja wa Shamba la Bibi ungejaa na hata hayo matatizo yasingetokea.
Na sio kwamba kukodi uwanja wa Taifa haiwezekani, ukweli ni kwamba inawezekana kwani matamasha kibao ya kidini ikiwemo ya Mkesha wa Pasaka na yale ya kufungia mwaka yamekuwa yakifanyika kwenye uwanja huo, ni suala la kubadilika tu.
Kingine cha kuwakumbusha watu wote wanaotarajia kutumia viwanja vya Leaders kwa matamasha au matukio makubwa. Viwanja hivyo vilitangazwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Mhe. Paul Makonda, kuwa mwisho wa kutumika ni saa 6 usiku.
Ruge kumtafuta RC Makonda kuhusu Fiesta mwisho saa 6 usiku
Pia kuna sababu nyingi zimekuwa zikitolewa na serikali, kwamba viwanja hivyo vipo karibu na Hospitali ya Ubalozi Medical Clinic, jambo ambalo linawabughuzi wagonjwawaliolazwa.
Kwa hiyo, ili matatizo hayo yasitokee tena, Waandaaji wa Matamasha mengine yanayokuja muandae njia mbadala kama mtahitaji kuvitumia tena viwanja vya Leaders.
Uwanja wa Taifa upo tunataka kuona watu wakijaa mule ndani kama nchi nyingine. Pia viwanja vya Tanganyika Packers vipo bado sioni sababu ya kung’ang’ania Leaders.
USHAURI KWA MAMLAKA HUSIKA:
Huu ni muda wa mabadiliko kwenye sanaa yetu, hivyo inatakiwa mchakato wa kupata vibali uwe mfupi, kusiwe na mlolongo mrefu ili kuendana na muda.
Sanaa yetu ni kazi na imekuwa mkombozi mkubwa kwa vijana, hivyo ni lazima tuendane na kasi ili kusongesha gurudumu la maendeleo ya Taifa letu.
Bongo5