Watanzania zaidi ya 1,400 wanatarajia kupata ajira za moja kwa moja kutokana na kampuni saba za Uturuki kuwekeza nchini.
Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Damas Ndumbaro alibainisha hayo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari juu ya ujio wa kampuni hizo.
“Ajira zaidi ya 1,400 zitapatikana endapo uwekezaji ukikamilika, lakini kuanzia mwaka 1990 hadi 2017 ajira zaidi ya 3,500 zimeshatengenezwa na kampuni za Uturuki 48 zilizokwishawekeza nchini zikiwa na thamani ya Dola za Marekani bilioni 324,” alisema Dk. Ndumbaro.
Alisema kampuni hizo zinakuja nchini kuwekeza kwenye viwanda vya pamba mkoani Simiyu kutokana na mkoa huo kulima pamba kwa wingi na kwamba zimevutiwa na juhudi zinazoonyeshwa na Mkuu wa Mkoa huo, Anthony Mtaka kwenye uwekezaji wa viwanda.
Dk. Ndumbaro alisema Waturuki pia watawekeza kwenye viwanda vya sukari, saruji, kuchakata mazao ya kilimo na kutengeneza vifaa vya ujenzi pamoja na kuwekeza katika sekta ya nishati.
Alisema wawakilishi wa kampuni hizo tayari wameshawasili nchini na leo watakuwa Kituo cha Uwekezaji (TIC) watakapokutana na wenyeji wao ambao ni Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Wizara ya Mambo ya Nje, Taasisi ya Sekta Binafsi, Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA).
Alisema wawekezaji hao pia watakutana na Mamlaka ya Ukanda wa Uwekezaji (EPZA), Shirika la Umeme (Tanesco) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).
Dk. Ndumbaro alisema mbali na kufanya uwekezaji kwenye viwanda, kampuni hizo pia zitajenga hoteli zenye hadhi ya nyota tano na maduka makubwa ya biashara jijini Dodoma.
Alisema uhusiano kati ya Tanzania na Uturuki ni wa kipekee na wa siku nyingi, akieleza kuwa mwaka 2009 nchi hiyo ilifungua ubalozi wake nchini na mwaka 2016, Tanzania ikafungua ubalozi Uturuki.
Alisema Tanzania imekuwa ikipeleka kwa wingi Uturuki mazao kama vile pamba, mbegu za mafuta, tumbaku na korosho.
Alisema idadi ya watalii wanaotoka Uturuki kuja Tanzania imekuwa ikiongezeka, akibainisha kuwa mwaka 2012, watalii 2,700 kutoka Uturuki walikuja Tanzania.
Alisema ujio wa kampuni hizo ni mwendelezo wa juhudi za Rais John Magufuli wa kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya viwanda na yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.