Makonda Ammwagia Sifa Lowassa, Amponda Kubenea

Makonda Ammwagia Sifa Lowassa, Amponda Kubenea
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema licha ya wabunge kuwatumia vijana kujipatia kura, wamekuwa nyuma katika kuhudhuria shughuli za msingi za maendeleo.

Makonda ameyasema hayo leo Jumanne Novemba 27, 2018 wakati wa uzinduzi wa maktaba ya kisasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 2,100 kwa wakati mmoja na kuhifadhi vitabu 800,000.

Akizungumza katika uzinduzi huo unaofanywa na Rais John Magufuli, Makonda amesema alitarajia kuona wabunge wakiunga mkono juhudi za  maendeleo zinazofanywa, lakini wamekuwa wakikaa bila kuonyesha kuguswa kwao.

"Hata yule mbunge wa Ubungo (Saed Kubenea-Chadema) ambaye chuo hiki kipo katika jimbo lake sijamuona, kwa kweli nampongeza sana (Waziri Mkuu wa zamani, Edward) Lowasa kwa sababu anaoneka kukubali juhudi zako unazozifanya," amesema Makonda.

Mbali na hilo, Makonda amesema kabla ya Desemba makazi yote katika Jiji la Dar es Salaam ambayo hayana hati yatapimwa na hati zake kukabidhiwa kwa wamiliki.

Naye makamu mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye amesema milango iko wazi kwa wanafunzi wa vyuo vingine kwenda kujisomea katika maktaba ya kisasa ili kujiongezea ujuzi.

Akielezea sifa za maktaba hiyo, Profesa Anangisye mbali na kudai ndiyo maktaba inayoongoza kwa ukubwa Afrika Mashariki na Kusini. Pia, Maktaba hiyo imeunganishwa na umeme jua kwa kiwango cha kilovolt 280 zenye uwezo wa kuwasha taa na viyoyozi.

"Maktaba hii ni muhimu katika maendeleo ya chuo chetu hasa kwa wataalamu wake kujielimisha kupitia tafiti zilizotangulia," amesema Profesa Anangisye.

Pia, amesema ujenzi wa maktaba hiyo umegharimu Dola 41,280 milioni za Marekani huku chuo kikitoa Sh1.78 bilioni kwa ajili ya kugharamia nakala za vitabu na majarida.

Pia, maktaba hiyo ina ukubwa wa kilomita za mraba 4.4 huku ikiwa na kompyuta 160 zinazowezesha wanafunzi kusoma vitabu kwa njia ya mtandao.

"Tunatambua michango ya hali na mali inayofanywa na ubalozi wa China nchini katika kusaidia mambo mbalimbali ya kijamii na kiuchumi chuoni  kwetu inayotuletea maendeleo," amesema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad