Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda amesema kuwa viongozi wa Upinzani mkoani mwake wamekuwa wakijitenga katika shughuli za maendeleo ikiwemo uzinduzi wa baadhi ya miradi.
Makonda ametoa kauli hiyo leo katika hafla ya uzinduzi wa maktaba mpya katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), ambapo amesema kuwa ameshangazwa na kutokuwepo kwa Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Saed Kubenea mahala ambapo Chuo kinapatikana katika Jimbo lake, pamoja na majirani zake ambao ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika.
"Nashangaa hata wale wabunge wapinzani wa Dar es salaam ambao mara nyingi wanakuja vyuoni kuwarubuni wanafunzi wawapigie kura lakini hawatokei kwenye shughuli za maendeleo, kazi yao ni kukosoa tu", amesema Makonda.
Aidha amesema kuwa wamekuwa wakijionesha kuwa ni wapiganiaji wa maendeleo kwa maneno na sio vitendo, huku akimpongeza Waziri mkuu wa zamani na mjumbe wa kamati kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edward Lowassa kwakuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono wa shuguli mbalimbali za maendeleo.