Mama Samia Aionya Takukuru Kukumbatia Wala Rushwa

Mama Samia

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ameionya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Rombo kutokana na taarifa kwamba baadhi ya maofisa wake wanatumika kuwalinda watendaji wa serikali wanaojihusisha na rushwa.

Samia alitoa onyo hilo jana akiwa katika sehemu ya ziara yake ya siku tano ya kikazi mkoani Kilimanjaro.

Alisema asilimia 90 ya watendaji wa serikali katika wilaya hiyo wanatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa wakati wakutoa huduma kwa wananchi, huku akiionyooshea kidole taasisi hiyo kwa kuwafumbia macho watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Rombo.

"Nasikitika kusema kuwa asilimia 90 ya watendaji wa halmashauri wanafanya kazi kwa kupokea rushwa ili kuwaudumia wananchi. Niwaonye na niwaambie taarifa hizo tunazo na majina yenu tunayo. Jirekebisheni mara moja kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa.

“Takukuru sidhani kama mnatambua wajibu wenu au nimeona jengo tu ambalo halina utendaji? Wananchi wengi wanashindwa kupata huduma na wanapiga simu kwenye ngazi za juu ili kuomba msaada na wanakiri kutoa pesa ili kutekelezewa jambo lao. Haipendezi na hii ni dhambi kubwa sana, jirekebisheni isiwe tu tuna taasisi jina," alisema.

Aliitaka taasisi hiyo kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi na kujitahidi kutunza siri kwa wananchi wote zinazotoa taarifa na kuhakikisha hatua kali za kisheria zinachukuliwa kwa watakaobainika kujihusisha na rushwa.

“Sisi tumewaweka hapo ili msaidie wananchi kupata haki zao kwa wakati na baadaye wapate nguvu ya kwenda kwenye majukumu yao na kuzalisha na badala yake mmekuwa chanzo cha chuki na ukandamizaji wa haki za wananchi, hatutakubali na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yenu,” alisema Samia.

Pia alisema katika halmashauri hiyo, suala la rushwa ya ngono kwa watendaji wa kiume na ubaguzi wakati wa uwajibikaji, limekuwa likishika kasi siku hadi siku.

Kuhusu uhusiano kati ya halmashauri hiyo na wananachi, Makamu wa Rais aliwataka viongozi na watendaji wa kuacha malumbano na badala yake washirikiane katika kuwahudumia wananchi

Alisema malumbano yanayotokana na itikadi za vyama vya siasa yanawacheleweshea wananchi maendeleo na kupoteza ari ya kuwajibika miongoni mwa watendaji wa ngazi ya chini.

“Hata kama umepewa kazi na mjomba wako, ukifika hakikisha unawajibika na kuwatumikia wananchi na si kuanzisha malumano na misuguano isiyo na tija. Hatutakuvumilia unapokwamisha maendeleo hayo,” alisema Samia.

“Mkishindwa kushirikiana maendeleo yatarudi nyuma na watakaoathirika si Rais (John Magufuli wala mimi bali ni wananchi ambao siku zote  wanatulalamikia kuhusu utendaji usio wa kuridhisha kutokana na kutokuelewana kwa baadhi ya viongozi”, aliongeza.

Akisoma taarifa ya wilaya, Mkuu wa Wilaya hiyo, Agnes Hokororo, alisema ziko  changamoto nyingi wanazokabilina nazo lakini kubwa zaidi ni maji hasa ukanda wa chini

“Tunaiomba serikali kuu kutufikiria namna ya kutusaidia wananchi wa ukanda wa chini wapate maji safi na salama kwa kipindi cha mwaka mzima,” alisema.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad