Mwanamke mmoja aitwaye Malagalita Mathias, (55) mkazi wa kijiji cha Nyatukala wilayani Sengerema, anashikiliwa na Polisi kwa kosa la kupatikana na pombe aina ya (gongo) kiasi cha lita 20 na dawa za kulevya aina ya mirungi kiasi cha kilo moja.
Tukio hilo limetokea jioni ya novemba 5 mwaka huu, baada ya kupatikana kwa taarifa kwamba katika Vijiji vya Nyamizeze na Nyatukala vilivyopo Wilayani humo wapo watu wanaojihusisha na uuzaji pamoja na utengenezaji wa pombe ya gongo na dawa za kulevya aina ya mirungi.
Akizungmza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Jonathan Shanna amesema “baada ya kupatikana kwa taarifa hizo Polisi ilifanya msako mkali katika vijiji hivyo na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa tajwa hapo juu akiwa na kiasi hicho cha pombe ya moshi (gongo) na mirungi huku wenzake wakifanikiwa kutoroka”.
Aidha amesema “polisi tunaendelea na mahojiano na mtuhumiwa ili kuweza kubaini wenzake anaoshirikiana nao katika biashara hiyo haramu ya gongo na mirungu, pindi uchunguzi ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani."
Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia mtuhumiwa wa utapeli aliyefahamika kwa jina la Benedicto Bahati, (29) mkazi wa kiloleli, kwa tuhuma za kujifanya afisa wa TCRA, kitendo ambacho ni kosa la jinai.