VIDEO inayosambaa inayomuonyesha muimbaji maarufu wa Injili, Rose Muhando akiwa anaombewa baada ya kupagawa na mapepo imeshtua wengi. Video hiyo inayomuonyesha Rose akiwa amedhoofu mwili wake huku akiwa na makovu kama ameungua moto ilisambaa kwa kasi jana kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii hali iliyosababisha Amani limtafute kwa njia ya simu lakini hakupatikana. Baada ya kugonga mwamba kwa Rose, paparazi wetu alimtafuta msemaji wake ambaye ni Mchungaji Daud Mashimo na kueleza ilivyokuwa.
“Ni kweli Rose anaumwa lakini anaendelea na huduma ya uimbaji ambapo kwa sasa yupo kwenye ziara nchini Kenya ambako ndiko alikokuwa akiombewa kama video inavyoonyesha. “Baada ya kuombewa na mapepo kulipuka kwa sasa anaendelea vizuri na baada ya kumaliza ziara Kenya, ataenda Uganda na atamalizia na Zambia,” alisema Mashimo.
Kutokana na kusambaa kwa video hiyo ambayo Rose amepandisha mapepo yanayozungumza kwamba hayataki aimbe tena na kumtaja aliyekuwa meneja wake, Nathan ndiye mbaya wake, Chama cha Muziki wa Injili (Tanzania Music Foundation) kimeibuka na kutoa kutoa tamko.
Akizungumza katibu mwenezi wa chama hicho, Stella Joel alisema wao kama chama wameingilia kati suala la Rose kwa ambaye kwa sasa yupo nchini Kenya na wamemtaka arudi nchini haraka. “Kama chama tumeamua kulishughulika hili suala la Rose maana kwenye ile video amemtaja Nathan ambaye ni meneja wake wa kitu ambacho kinaonyesha picha mbaya.
“Tumemwambia Rose arudi haraka nchini maana yupo Kenya amehifadhiwa na mwimbaji mwenzake, ambapo na meneja wake huyo Nathan atakuja Dar kwa ajili ya kuzungumzia madai aliyotoa maana tunaamini pale siyo mapepo bali kuna mchezo Rose anaucheza,” alisema Stella. Stella alieleza kuwa ni kweli Rose afya yake ni dhoofu na anaumwa hivyo wameshawatafuta madaktari kutoka Hospitali ya Apollo nchini India ambao wako hapa nchini tayari kwa ajili ya kushughulikia maradhi yanayomsumbua Rose.