Maradona amesema kuwa Jose Mourinho ndiye kocha bora ukilinganisha na Pep Guardiola ambaye anatumia faida ya ufundi aliokuwa nao kutoka kwa mchezaji na kocha wa zamani wa Barcelona, Johan Cruyff.
Guardiola aliiongoza City msimu wa ligi kuu uliopita na kufanikiwa kunyakua taji la EPL, na timu yake imerudi tena vizuri kwenye kampeni ya msimu huu, wakati Mourinho na Man United wakijitahidi kutoka katika hali ngumu iliyonayo hivi sasa, baada ya kupigwa katika mchezo wa 'derby' siku ya Jumapili.
"Kwangu mimi ndiyo, Mourinho ni bora, napenda kumpa sifa Pep Guardiola kwa kutumia faida ambayo Johan Cruyff alimpa. Nimesema kwa zaidi ya tukio moja kwamba tiki-taka haijatengenezwa na Guardiola, ilikuwa ni ya 'Flaco' Cruyff, " amesema Maradona.
"Kwa sasa Pep anaweza kuchagua mchezaji yeyote duniani ambaye anamtaka. Kwa njia hiyo tiki-taka ni rahisi," ameongeza.
Alipoulizwa kama atakuwa na nia ya kufundisha nchini Hispania, Maradona ambaye ni mshindi wa Kombe la Dunia mwaka 1986 alisema tu "ni mradi wa muda mrefu" akihitajika, lakini kwanza anataka kwenda Manchester United kujifunza kutoka kwa Mourinho.
"Mimi mwenyewe kama kocha ninahitaji kujifunza mengi na kwa sababu hiyo nadhani nitakwenda Manchester na Mourinho kumwomba mambo mengi," amesema Gwiji huyo wa Argentina.