Marekani imetangaza kuwa leo Nov 5 imeirejeshea vikwazo nchi ya Iran vitakavyolenga sekta ya mafuta na sekta ya kifedha.
Marekani imesema imeiwekea Iran vikwazo vigumu zaidi ambavyo haijawahi kuiwekea. Vikwazo hivyo vitalenga mauzo ya mafuta, usafiri kwa njia ya baharini na mabenki ambavyo vyote ni muhimu sana kwa uchumi.
Maelfu ya raia wa Iran wakiwa na mabango yaliyoandikwa "Kifo kwa Marekani" wameandamana wakiitaka serikali yao kutofanya mazungumzo yoyote na Marekani.
Jeshi la Iran nalo limesema kuwa litafanya mazoezi ya kijeshi leo Jumatatu na Jumanne kuonyesha uwezo wake wa kijeshi.
Marekani imetangaza vikwazo hivyo baada ya Rais Trump kutangaza kujitoa kwenye mkataba wa mwaka 2015 uliolenga kupunguza mipango ya nyuklia ya Iran.
Marekani inasema inataka kuzima vitendo viovu vya Ina vikiwemo udukuzi wa mitandao, majaribio ya makombora ya masafa marefu na uungaji mkono wa makundi ya kigaidi mashariki ya kati.
Zaidi ya watu 700, kampuni, vyombo vya habari na ndege kwa sasa vimewekewa vikwazo, yakiwemo mabenki makubwa, wauza mafuta na kampuni za usafiri wa baharini.
Wakati hayo yakijiri, Uingereza , Ujerumani na Ufaransa ambazo ni kati ya nchi zilizo kwenye makubaliano ya nyuklia zote zimekataa vikwazo hivyo vya Marekani dhidi ya Irani.
Zimeahidi kuzisaidia kampuni za Ulaya zinazofanya baishara halali na Iran na kubuni njia mbadala za malipo ambazo zitasaidia kampuni kufanya bishara bila ya vikwazo vya Marekani