Mawaziri Waliotumbuliwa na JPM Waongezeka
0
November 11, 2018
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, jana Novemba 10, 2018, alitengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara Charles Mwijage na Waziri wa Kilimo Dkt Charles Tizeba.
Nafasi ya Dkt Charles Tizeba imeshikwa na Japhet Hasunga, ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii huku nafasi ya viwanda na biashara iliyokuwa chini ya Charles Mwijage, imechukuliwa na Joseph Kakunda, ambaye naye kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali Mitaa TAMISEMI.
Kufuatia mabadiliko hayo madogo ya baraza la mawaziri, sasa inafanya idadi ya mawaziri waliotumbuliwa katika uongozi wa awamu ya tano chini ya Dkt. John Magufuli kufikia sita. Mawaziri wengine waliotumbuliwa kabla ya mabadiliko ya jana ni kama ifuatavyo hapo chini.
Waziri wa kwanza kabisa kutumbuliwa ni Charles Kitwanga ambaye Rais Magufuli alitengua uteuzi wake Ijumaa, Mei 20, 2016 baada ya kuingia bungeni kujibu swali linalohusu Wizara yake akiwa amelewa, ikiwa ni siku chache tu baada ya kuwasilisha bajeti ya Wizara yake ya Mambo ya Ndani ya Nchi ya 2016/17.
Mnamo Machi 23, 2017, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye na nafasi yake kuchukuliwa na Dkt. Harisson Mwakyembe ambaye anahudumu katika nafasi hiyo hadi hivi sasa.
Tarehe 24, Mei, 2017 Rais John Magufuli alimfuta kazi aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo wakati akipokea taarifa ya kamati maalum aliyoiunda kuchunguza mchanga wa madini uliokuwa katika makontena zaidi ya 200 aliyoyazuia yasisafirishwe, kwa ajili ya uchunguzi.
Pia, Rais Magufuli alimfuta kazi aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Mwigulu Nchemba, Julai Mosi, 2018 na nafasi yake ikichukuliwa na Kangi Lugola ambaye alikuwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira.
Waziri mwingine ambaye alitolewa katika nafasi yake ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Susan Alphonce Kolimba mnamo Septemba 26, 2018 ambapo nafasi yake ikichukuliwa na Dkt Damas Daniel Ndumbaro ambaye ni Mbunge wa Songea Mjini Mkoani Ruvuma.
Tags