Alidai alikwenda kumueleza malalamiko ya wananchi kuhusu amri ya Mkuu wa Wilaya ya Moshi ya kusitisha ujenzi wa barabara na kusababisha hasara ya mabilioni ya shilingi.
“Haya yote nimemueleza Mheshimiwa Rais (Magufuli) niwe mkweli, nilibahatika hapo katikati Mheshimiwa Rais akaniita akasema hivi, narejea sauti ya Rais aliniambia na ameshaagiza ofisi zake na wengine wameniita Dodoma, barabara za wana Vunjo atachangia yeye binafsi kama John Pombe Magufuli, pili serikali yake itachangia na tatu atakuja kama Amiri Jeshi Mkuu kufungua barabara hizi yeye mwenyewe kama John Pombe Magufuli,”alisema
Mbatia alikuwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Makuyuni katika Mamlaka ya Mji mdogo wa Himo, Wilaya ya Moshi wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya ghalani.
Mradi wa upanuzi na ujenzi barabara za vijijini kwa kiwango cha changarawe unaodaiwa kusisitishwa katika Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, unahusisha barabara zenye urefu wa kilometa 389.3 ambazo zilikuwa zigharimu Sh. bilioni 12.077 kutokana na utafiti wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) wa mwaka huu.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi Warioba anadaiwa kusimamisha kazi ya ujenzi wa barabara hizo na hivyo kusababisha hasara.
Zaidi Mbatia alisisitiza: “Sasa tuone ni nani zaidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na maendeleo ya watanzania, maendeleo hayana itikadi za vyama. Kwa nini amefanya hivyo, kwa sababu Jimbo la Vunjo tumekuwa wa kwanza Tanzania kuweza kujipanga wenyewe mpaka hatua tuliyofikia ya kujiletea maendeleo yetu wenyewe na tujipongeze wana Vunjo.
"Hizi barabara zikiwa vizuri si tunazitumia sote, barabara za Makuyuni zikiwa nzuri zitaendelea kutumiwa na watu wote hata kama Mbatia sitakuwa Mbunge…Mimi sijawahi kumtukana Rais, sasa atakuja yeye mwenyewe.”
Mbatia alikutana na Rais Magufuli na kufanya mazungumzo naye Ikulu, Novemba 13 mwaka huu akiwa pamoja na wanasiasa wengine Mh. John Cheyo (UDP), John Shubuda na mfanyabiashara Rostam Aziz.
Katika mkutano huo, Mbatia aliwaeleza wananchi hao kwamba amekopa fedha zaidi ya Sh. milioni 500 Benki ya CRDB kwa ajili ya kununua mitambo ya ujenzi wa barabara hizo.
“Mimi nimenunua mitambo sawa, mingine tunakodisha sawa lakini tukasema wananchi waanze kuchangia mafuta kwenye hiyo mitambo hiyo, kwa mfano Kijiji cha Mshihiri mpaka leo hii wameshachangia takribani Sh. milioni 26 lakini ukichanganya zote pamoja na za Ashira ni zaidi ya Sh. milioni 30 na kitu huko,”alieleza
Akijibu maswali ya wananchi kuhusu kukwama kwa ujenzi wa barabara za Samanga/Sembeti, Mbunge huyo alisema Mungu sio Athuman na akawataka wananchi hao kusubiri kwanza ili mdomo wake usiteleze kwa vile wana kesi mahakamani.
Wakati anahitimisha mkutano huo, Mbatia aliipongeza Kamati ya Maendeleo ya wana Vunjo (VDF) chini ya Askofu Mstaafu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Dk. Martin Shao, mashekhe wetu, mapadri wetu na wachungaji na viongozi wote, akisema yeye binafsi toka sakafu ya moyo wake hana chuki na mtu yeyote na anamshukuru Mungu amesikia na Mheshimiwa Rais (Magufuli) amesikia dua zao.