KOCHA Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Patrick Aussems ameweka wazi kuwa hana mpango wa kuifuatilia kasi ya Yanga kwa kuwa sasa wanalingana pointi lakini amefichua kuwa imemsaidia kupunguza presha ya mechi zake kutokana na kufikiria kutetea ubingwa wao kwani bado wanaendelea kupiga hesabu zao.
Licha ya Azam FC kuongoza katika msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa kuwa na pointi 30, lakini nyuma yao wapo Simba wanaoshika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 26, sawa na Yanga wanaoshika nafasi ya tatu japokuwa Simba wana mchezo mmoja zaidi ya Yanga.
Mara baada ya mazoezi ya timu yake juzi, Uwanja wa Boko Veterani, Aussems alipata nafasi ya kuzungumza na Championi Ijumaa na kusema kuwa sawa na Yanga katika msimamo wa ligi kuu kumempunguzia presha kutokana na ushindani wa ligi ilivyo, kwani sasa wanachokiangalia ni kuweza kutetea ubingwa wao.
“Sawa Yanga tupo juu yao lakini presha kwa kiasi fulani imeshuka kwa sababu wao wamekuwa wakifanya kazi yao, sare dhidi ya Ndanda kwao ni faida kwetu kwa kuwa tunatakiwa kuangalia mbali.
“Lakini hili siyo jambo la kutegemea maajabu kwamba kesho itakuwaje au nitakuwa wapi lakini naangalia zaidi kwenda mbali zaidi ya hapa na hilo ndiyo lengo lilivyo, hata kwa upande wa wachezaji kwa sababu hatuhitaji kuona tunashindwa licha ya ushindani wa maadui ulivyo kwa kuwa mwisho wa siku tupate ubingwa,” alisema Aussems.