VIONGOZI watatu wa Chama cha Wananchi (CUF) leo Ijumaa, Novemba 23, 2018 wameachiwa, baada ya kukamilisha masharti ya dhamana, yaliyowekwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Lindi.
Walioachiwa ni pamoja na Naibu Mkurugenzi wa Habari na uwenezi Taifa, Mbalala Abdallah Maharagande,M’bunge wa Jimbo la Kilwa Kusini, Selemani Said Bungala (Bwege) na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Abuu Mussa Mjaka.
Viongozi hao walilazimika kurejeshwa mahabusu jana kufuatia baadhi ya barua za wadhamini kukosew majina na muda wa kazi za ofisi kumalizika wakati hawajakamilisha taratibu za dhamana zao.
Hata hivyo dhamana ya viongozi hao, ilitaka kuingia dosari kwani hadi saa 5:16 asubuhi, walikuwa bado hawajafikishwa Mahakamani kwa madai mbalimbali, ikiwemo kukosekana kwa askari wa kuwafuata gerezani, na kufanikiwa kuletwa saa 7:45 na kukamilika kwa taratibu ndogondogo za ki-Ofisi, ambapo wameachiwa saa 9:30 Alasiri.
Aidha,Viongozi hao wanakabiliwa na mashitaka matano, yakiwemo mawili ya kuuwa, pamoja na kutoa lugha ya uchochezi na matusi, wakati wa mkutano wa uzinduzi wa uchaguzi mdogo wa udiwani, uliokuwa umefanyika viwanja vya Maalimu Seif Gurden uliopo mji mkongwe wa Kivinje.
Wakili anayewatetea viongozi hao, Rainery Songea, akizungumza mara baada ya kukamilika kwa taratibu hizo, alisema uwepo wa kesi hiyo haitawazuia kujihusisha na shughuli zozote zinazohusiana na kampeni inayoendelea hivi sasa.
Aidha, Wakili Songea ameendelea kuwasisitiza wateja wake, kuzingatia Sheria na taratibu zilizowekwa na Tume ya uchaguzi wanapoendesha mikutano yao ya kampeni.
Shauri la washitakiwa hao namba 10 na 11/2018, limepangwa kufikishwa tena mbele ya Mahakama hiyo, Decemba 3, mwaka huu, na hivyo kurejea majumbani mwao kuendelea na majukumu yao.