MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu leo imeahirisha tena kesi inayomkabili mfanyabiashara Akram Aziz Abdul Rasool ya utakatishaji fedha wa Dola za Marekani 9,018 kwa kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Wakili wa Serikali, Elia Athanas, akiieleza mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Augustine Rwezire, alisema kuwa shauri hilo liliitishwa kwa ajili ya kutajwa ambapo wakili Athanas amedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo anaomba kesi iahirishwe.
Baada ya kueleza hayo kesi imeahirishwa hadi Novemba 26, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande.
Akram ambaye ni mdogo wa aliyekuwa mwanasiasa na mafanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz, anakabiliwa na mashtaka 75 katika kesi ya uhujumu uchumi namba 82/2018 ambapo katika makosa yake, mawili ni kukutwa na nyara za serikali, kukutwa na silaha na utakatishaji fedha.
Kuhusu kukutwa na nyara za serikali, inadaiwa alitenda kosa hilo Oktoba 30, 2018 maeneo ya Oyster Bay, Dar es Salaam, ambapo alikutwa na meno sita ya tembo yakiwa na thamani ya Sh. mil. 103.
Pia anashitakiwa kwa kukutwa na nyama ya nyati, kilo 65 yenye thamani ya Sh. mil. 4.35 ikiwa haina kibali, kosa alilolitenda Oktoba 30,2018 maeneo ya Oyster Bay, Kinondoni, Dar es Salaam.
Pia anakabiliwa na kosa la kukutwa na risasi 2,404, kosa ambalo alilitenda Oktoba 30,2018 maeneo ya Oyster Bar Dar es Salaam ambapo kosa jingine ni kukutwa na silaha aina ya bastola, kosa alilolitenda Oktoba 30,2018 maeneo ya Oyster Bay, Dar es Salaam, ambapo silaha hiyo haikuwa na kibali cha mrajisi wa silaha.