Upelelezi wa kesi inayomkabili mfanyabiashara Akram Azizi ambaye anakabiliwa na mashtaka 75 ya uhujumu uchumi kwa kukutwa na nyara za Serikali, silaha aina mbalimbali na risasi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu bado haujakamilika.
Wakili wa Serikali Mtalemwa Kisheny leo Jumatatu Novemba 26, 2018 amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Augustine Rwizile kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kwamba kesi ilipangwa kwa ajili ya kutajwa.
Wakili wa utetezi Saidi Maliny amedai kwa rekodi ya jalada na kasi waliyokuwa nayo alitegemea upande wa mashtaka watakuwa wamekamilisha upelelezi.
"Upande wa mashtaka watoe dira ya upelelezi ili mtuhumiwa aweze kujua kesi inaanza kusikilizwa lini" amedai Wakili Malinyi.
Wakili wa Serikali Kisheny amedai baada ya kukamilika kwa upelelezi kesi hiyo itaenda Mahakama Kuu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa kwa kuwa kesi hiyo ni ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha.
Baada ya kueleza hayo Hakimu Rizwile ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 6, 2018 na mshtakiwa huyo amerudishwa rumande.
Mbali na mashtaka hayo, Azizi pia anakabiliwa na shtaka la kutakatisha fedha kiasi cha Dola 9018.
Katika kesi hiyo anakabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa na nyara za Serikali zenye thamani ya Sh108 milioni, risasi 6,496 bila ya kibali kutoka kwa mrajisi wa silaha.
Pia anakabiliwa na kosa la kukutwa na nyama ya nyati kilogramu 65 yenye thamani ya Sh4.35 milioni bila ya kuwa na kibali kutoka kwa mkurugenzi wa wanyamapori.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Oktoba 30 na 31, 2018 huko Oysterbay Kinondoni, Dar es Salaam.
Katika shtaka la utakatishaji mshtakiwa anadaiwa kati ya Juni 2018 na Oktoba 30, 2018 katika eneo la Oysterbay, alijipatia Dola 9,018 huku akijua kuwa kiasi hicho cha fedha ni zao la kosa tangulizi la kujihusisha na biashara haramu ya nyara za Serikali pamoja na kukutwa na silaha bila kibali.
Mshtakiwa huyo anaendelea kusota rumande kwa sababu miongoni kwa mashtaka yanayomkabili, shtaka la utakatishaji fedha ni miongoni mwa mashtaka kwa mujibu wa sheria na hayana dhamana.