Mhasibu aswekwa 'Lock Up' saa 48 kisa EFDs
0
November 03, 2018
Mhasibu wa Mapato wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Salutare Mlay, amejiingiza kwenye 18 za Mkuu wa Wilaya hiyo, Lengai Ole Sabaya, ambaye ameagiza awekwe mahabusu ya polisi kwa saa 48 kwa kosa la kutoa mashine tano za risiti za kielektroniki (EFD) kwa watu ambao hawawezi ..
Mlay alikumbana na balaa hilo la kwenda kulala ‘lock up’ kwa siku mbili mfululizo kuanzia jana saa 3:30 asubuhi, muda mfupi baada ya kufika katika Ofisi ya Mkuu huyo wa Wilaya ambaye aliamuru apelekwe moja kwa moja Kituo Kikuu cha Polisi Bomang’ombe.
Mhasibu huyo anatuhumiwa kuwapa mashine hizo, watu ambao hawana utaalamu wa ukusanyaji wa mapato yatokanayo na madini ya mchanga unaochimbwa katika wilaya hiyo, huku wakitoza 7,000 na kupeleka fedha kiduchu katika halmashauri hiyo.
“Afande, huyu aende 48 kwanza, amechukua mashine za EFD amewapa watu ambao hawana utaalamu wa ukusanyaji wa mapato ya halmashauri. Huko wanakusanya mapato yatokanayo na madini ya mchanga, lakini ukiangalia yale makorongo wanayochimba mchanga yanataka kuanguka saa yeyote.
Zaidi alisema: “Wanatoza Sh. 7,000 kwa lori, jana kwa mfano walikusanya lori zaidi ya 30 kwa siku, lakini hapa halmashauri kwa wiki wanaleta Sh. 150,000. Kwa hiyo huyo (Mlay) sehemu yake salama ni huko, hakuna mjadala.”
Jana wakati alipokwenda kukagua machimbo hayo, Sabaya alisitisha shughuli zote za uchimbaji wa madini ya mchanga kwenye wilaya hiyo, hadi hapo uchunguzi utakapokamilika kuhusiana na utaratibu uliotumika katika utoaji wa vibali vya uchimbaji pamoja na ukusanyaji wa mapato.
Mkuu huyo wa wilaya alifikia uamuzi wa kusimamisha shughuli hizo, baada ya baadhi ya maswali yake kukosa majibu.
Pamoja na mambo mengine, Ofisa Mazingira wa Wilaya hiyo, Alfred Njegite, akizungumza mbele ya Sabaya alisema shughuli za uchumbaji wa madini ya mchanga kwenye machimbo hayo siyo rafiki na mazingira, huku zikiibua hofu juu ya usalama wa wachimbaji wadogo kwenye machimbo hayo.
Kadri miaka inavyokwenda tatizo la uchimbaji mchanga linaonekana kuwa kubwa, huku kukiwa hakuna hatua za haraka kukomesha hali hiyo.
Tags