Miaka 3 ya Rais Magufuli Madarakani, Wapinzani Wapo Mahututi Hawana Hoja

Ilikua ni Novemba 5, 2015 pale Rais mteule wa Tanzania Mh.Dr.John Pombe Joseph Magufuli alipoapishwa katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar Es Salaam na hivyo kuwa rasmi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nchi ilikua imetoka kwenye zoezi gumu la Uchaguzi mkuu ambao ulipandisha sana joto la kisiasa. Wapinzani walikua wanaugulia maumivu baada ya kupokea kichapo kikali, na wakawa wanajipanga kuibuka na hoja zitakazowasaidia kuwaweka tena kwenye ramani ya kisiasa baada ya kushindwa uchaguzi.

Mara baada ya kuingia ofisini Rais Magufuli akaanza kuipanga na kuinyoosha nchi kwenye masuala kadhaa ambayo yalikua ni ugonjwa wa Taifa kama upotevu wa mapato uliokua unafanyika TRA na Bandarini.Rais Magufuli akaanza kuirejesha nchi kwenye misingi kwa maneno mengine alianza kuirudisha treni kwenye reli yake.
Hatua hiyo ya uchapaji kazi wa Rais Magufuli ukawa ndio mwanzo wa wapinzani kuanza kutapa tapa,kudhoofu na mpaka kufikia leo hii wapo mahututi.

Tuangazie maeneo kadhaa ambayo ambayo yamesababisha wapinzani kuwa mahututi kisiasa.

UWAJIBIKAJI
Hatua hii imepelekea upinzani kwa mahututi kabisa.Serikali ya awamu ya 5 chini ya uongozi wake Mh.Magufuli imejipambanua kuwa ni Serikali yenye kuwajibika kwa maslahi mapana ya Watanzania.
Mashirika ,Idara na ofisi nyingine za umma kote huko ni mchakamchaka wa kuwahudumia wananchi,vitendo vya uzembe na uvivu kwenye ofisi za Serikali vimepungua kwa kiasi kikubwa.Sasa ni kazi tu.

MAPAMBANO DHIDI YA UFISADI, RUSHWA, NA UHUJUMU UCHUMI
Wapinzani walitumia ufisadi rushwa na uhujumu uchumi kama ganda la ndizi la kutelezea katika kutafuta kukubalika na kujenga umaarufu wa vyama na wanasiasa wao kwa Wananchi.Mara baada ya kuapishwa Rais Magufuli akayavalia njuga masuala hayo ,akayakamua mafisadi kutoka kila pembe ya nchi habari zikavuma kusini na kaskazini.
Kwa mara nyingine wapinzani wakanyanga'nywa hoja MAMA waliyokua wanaitegemea .

ULINDAJI WA RASLIMALI ZA TAIFA
Rais Magufuli kwa kutambua kwamba nchi yetu imebarikiwa Raslimali nyingi na ambazo kama zikipata usimamizi mzuri zinaweza kuipeleka Tanzania ,yenye uchumi wenye nguvu na kuwa nchi mfadhili (Donor Country),akaanza kuchukua hatua za dhati na za makusudi kabisa katika kuhakikisha kwamba kila Raslimali inalindwa dhidi ya wezi na maharamia, lakini pia inawanufaisha wenye nchi.
Hatua hii ikawa ni pigo kuu tena jingine kwa wapinzani wakawa wanaweweseka kwa kukosa agenda za maana.

UBORESHWAJI WA HUDUMA ZA JAMII
Magufuli amejipanga vizuri katika kuboresha huduma za jamii kwa watu wake.Afya, Miundombinu,Maji,Nishati Elimu kote huko kumefanyika mageuzi makubwa yaliyoleta furaha kwa wananchi. Hivi ninavyoandika Muhimbili wanapandikiza Figo.Wapinzani waliokua wanatumia uduni wa huduma hizo kama mitaji yako ya kisiasa wakawa wameachwa mataa Rais Magufuli akazidi kuchanja mbuga.

KUTETEA MASLAHI YA WANYONGE
Rais ndani ya miaka hii mitatu ameweza kwa kiasi kikubwa kushughulika na changamoto mbalimbali walizokua wanakutana nazo watu wa kipato cha chini kwa jina maarufu.Dhamira yake ya dhati ya kutaka watu kutoka katika tabaka hilo kufurahia Utanzania wao limeonekana hata kwa yeye mwenyewe kujiita ni Rais wa wanyonge .

Wakaanga vitumbua, wauzambogamboga,machinga,Bodaboda na wajasiriamali wengine wadogo wote hao kwa ujumla wao Rais Magufuli amewapa nafasi kubwa ya kupata haki zao na kufanya biashara zao.
Tulizoea hapo nyuma kidogo wapinzani kuyatumia makundi hayo hususani wamachinga kufanya maandamano yasiyo na tija lakini siku hizi wamachinga hawadanganyiki wameungana na Rais kwenye kuchapa kazi na wameachanaa na wapinzani wababaishaji waliokua wanawatumia kama makarai.

UFUFUAJI WA SHIRIKA LA NDEGE
Walipiga kelele wee inakuwaje nchi kama Tanzania haina hata kandege kamoja .Mara tu baada ya kuingia madarakani Rais Magufuli akanunua ndege mpya si mpigo tena kwa fedha taslimu(Cash Money)
Ndege zetu zimewasili na zinakata mawingu kila siku.Hoja ya ndege ikazimika wapinzani wakazidi kuparalaizi.

Kwa sasa ATCL imetawala soko la ndani kwa zaidi ya asilimia 24 ikisafirisha abiria katika mikoa 12 na katika nchi za Comoro, Burundi na Uganda.Vilevile shirika hilo limefanikiwa kuongeza mapato hadi Sh4.5 bilioni kwa mwezi.

KUIFANYIA MAGEUZI CCM (CCM MPYA)
Ilikua ni majira ya mvua za masika mnamo Machi 12 mwaka 2017 ambapo wajumbe wa mkutano mkuu maalumu wa CCM walipojichimbia pale Jijini Dodoma na kuamua kwa kauli moja kukifanyia chama hicho mageuzi makubwa ya kiuongozi,Kimfumo na Kiutendaji.
Mageuzi haya yalisimamiwa na Mwenyekiti Ndugu Dr.John Pombe Magufuli shabaha yake ni kuleta tija,ufanisi ,kukirudisha chama kwenye misingi yake, kuifanya CCM kiwe chama cha wanachama na kushughulika na shida za watu kikamilifu.
Hakika mageuzi haya ni mwiba mkali kwa wapinzani kwani yameongeza wanachama wengi,imani ya wananchi kwa CCM imerudi chama kimepata mvuto wa ajabu sasa hivi kila mtu anatamani kuwa mwanachama wa CCM.

Matokeo yake vyama vya upinzani vimebaki kwa vyama vya viongozi pekee na vya mitandaoni wanachama wao wengi wamewakimbia, hakuna mtu mwenye hamu na siasa za upinzani Tanzania siku hizi mambo yote yapo CCM.

UJENZI WA VIWANDA
Sera ya ujenzi wa Tanzania ya viwanda yenye uchumi wa kati iliasisiwa na Rais Magufuli.Wapinzani kama kawaida yao wakatoa maneno mengi ya kebehi juu ya Sera ya Tanzania ya viwanda.(Industrialization)

Lakini husda zao zimeshindwa kwani kwa kipindi ambacho Serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani, chini ya uongozi mahiri wa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, hadi Machi
2018, viwanda vipya 3,306 vimejengwa na vimetoa ajira nyingi za moja kwa na zisizo za moja kwa moja kwa Watanzania
Hii ikamaanisha kwa mara nyingine tena wapinzani wakakosa hoja ya kuongea kwenye sekta hiyo.

Kunyauka,kudhoofu,kudumaa na hatimaye kuwa mahututi kwa wapinzani hapa Tanzania kumesababishwa na na kasi ya Magufuli katika kuchapa kazi.Wamekosa eneo la kimjadala la kuanzisha hoja zenye mashiko.

Wameishia kudandia matukio na kuvunja sheria kwa makusudi ili wakamatwe angalau wapate kuandikwa kwenye magazeti.
Mageuzi makubwa mazuri anayoyafanya Rais Magufuli ndio sababu haswa ya upinzani kufifia na natabiri mwaka 2020 Rais Magufuli atapitwa bila kupingwa.

Augustino Chiwinga
0659438889
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad