Miili ya wanajeshi watatu ambao walikuwa ni walinzi wa amani katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na Jamhuri ya Afrika ya Kati inaagwa leo katika hospitali ya jeshi ya Lugalo baada ya kupokelewa katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere.
Taarifa iliyotolewa na jeshi hilo la wananchi wanajeshi hao waliofariki inasadikika kuwa walishambuliwa na kikosi cha waasi kwenye nchi hizo, majina yao ni Koplo Mohamed Mussa, Koplo Erick Masauri John pamoja na Praiveti Musa Shija Machibya.
Heshima za mwisho kwa mashujaa hao zitatolewa katika eneo maalum la kuaga miili ya marehemu katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo leo tarehe 23 Novemba 2018 kuanzia saa 2.30 asubuhi.
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limekuwa likishiriki mara kwa mara kwenye ulinzi wa amani katika nchi mbalimbali barani Afrika na duniani kwa kuratibiwa na shirika la umoja wa Mataifa UN, Umoja wa nchi za Afrika AU, au SADC.
Mwezi Disemba mwaka jana takribani wanajeshi 14 wa Tanzania ambao walikuwa walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa waliuawa katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kufuatia tukio hilo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guteress, alitangaza Umoja wa Mataifa kufanya uchunguzi wa tukio hilo la kuuawa kwa waliokuwa wanajeshi kadhaa walinda amani nchini Congo ambao wengi wao walikuwa ni watanzania.