BAADA ya hivi karibuni ndoa yao kudaiwa kuota mbawa, mwanamuziki wa kitambo, Hamis Ramadhan Baba ‘H.Baba’ ameibuka na kueleza kuwa Mbongo Fleva, Abdulaziz Chende ‘Dogo Janja’ ukipenda waweza kumuita ‘Janjaro’ siyo chaguo la mwanamama Irene Uwoya ndiyo maana wameshindwana.
H.Baba ambaye zamani amewahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Uwoya ameiambia Risasi Vibes kuwa, wawili hao wasingeweza kudumu kwenye ndoa kwa sababu mwanamama huyo chaguo lake lilikuwa ni Ndikumana pia anapenda wanaume warefu wenye nguvu na miili ya mazoezi.
Mwanamuziki huyu amezungumza mengi ikiwa ni pamoja na kuhusiana na muziki wake, ungana naye hapa chini kwa mahojiano zaidi.
Risasi Vibes: Kwanza kabisa mashabiki wanataka kujua kwa nini uko kimya sana kimuziki, umeacha?
Baba: Sijaacha muziki bali ninajiandaa kutoa kazi mpya.
Risasi Vibes: Unatarajia kutoa lini na umejipangaje sokoni maana kwa sasa wanamuziki ni wengi na ushindani ni mkubwa sana?
Baba: Wanamuziki kweli ni wengi ila wanafanana uimbaji mpaka uchezaji ila kumpata kama H.Baba bado hajapatikana kabisa maana mimi nafanya muziki aina ya Bongo Bolingo Fleva ambao ni tofauti kabisa na hao wanamuziki wa sasa wenye mashabiki bendera fuata upepo.
Risasi Vibes: Unauonaje muziki wa sasa na unafikiri kwa nini haudumu kama ule wa zamani?
Baba: Muziki wa sasa ni mzuri ila haudumu kwa sababu utunzi wake una matusi sana na vina vya mashairi yao ni majina ya watu maarufu tu kwa staili hiyo muziki huu baadhi ya wasanii wameuharibu kabisa, inauma ila kila mtu abebe msalaba wake.
Risasi Vibes: Unazungumziaje wasanii wanaoendesha sanaa kwa kiki?
Baba: Kwa upande wangu naona wapo sawa kwa sababu mashabiki wanataka umbea muda wote na kusemana hovyo hivyo kiki ndiyo habari ya mjini, mitandao kama Instagram ndiyo ofisi za wasanii.
Risasi Vibes: Nini madhara ya hizo kiki?
Baba: Kila chenye faida kina na hasara yake, madhara ya kiki ni kwamba nyimbo zinakufa, utunzi bora umepotea kabisa ndiyo maana wasanii wa sasa utunzi wao wa mstari wa kwanza wanamaliza na majina ya watu maarufu.
Risasi Vibes: Wewe upo ndani ya ndoa na msanii mwenzako, Flora Mvungi ambaye ulimbadili dini na anajulikana kwa jina la Khadija, unamuonaje Diamond (Platnumz) ataoa mwanamke wa aina gani maana amekuwa akitajwa na wanawake tofauti kila kukicha?
Baba: Kwanza nampongeza Diamond kwa sababu kupitia hao wanawake amejikuta akiongeza umaarufu
hasa mitandaoni sababu wanawake wa sasa na wao wanapenda kiki hivyo na wengine wanaoweza kuiga waige kibiashara ni nzuri.
Kuhusu kuoa, Diamond atafikia hatua ataoa kati ya wadada ambao watu hawataamini.
Risasi Vibes: Umesema Diamond ataoa mwanamke ambaye watu hawataamini, je, unafikiri atakuwa wa aina gani?
Baba:Naona yupo mtu sahihi kwake na huyo mtu siyo mtu wa kiki kabisa nahisi atatokea Zanzibar na ni mke bora siyo bora mke, nahisi atatulia. Kama mimi niliamua kutulia kwa Khadija (Flora) wangu Uwoya angenitema kama Dogo Janja ningeumia sana yaani ningeandamana kutoka Dar mpaka Mwanza kwa miguu maana mke anauma sana.
Risasi Vibes: Kwa hiyo unashukuru hukumuoa Uwoya maana angekutema?
Baba: Hapana Uwoya pia angekuwa kwangu angetulia tu ila kipindi kile wote tulikuwa watoto kiakili lakini kwa sasa amekua anajua maisha ni nini na mimi pia nishakua ila chaguo langu ni Khadija.
Risasi Vibes: Je, Uwoya ni chaguo sahihi kwa Dogo Janja?
Baba: Hapana, Uwoya chaguo lake lilikuwa ni Ndikumana ila Mungu alimpenda zaidi, kwa Janjaro sidhani kama atamuweza maana Uwoya anapenda wanaume warefu wenye nguvu na miili ya mazoezi.
Risasi Vibes: Unamshauri nini Dogo Janja kwa sasa baada ya kumwagana na Uwoya?
Baba: Namshauri akomae kama ataweza ukomavu kurudisha penzi ila Uwoya ana maamuzi yake binafsi akisema sikutaki ndiyo kamaliza.
Risasi Vibes: Una nini cha kumwambia msanii mwenzako Wema Sepetu kuhusiana na majanga yaliyompata ambapo kesi inaendelea mahakamani?
Baba: Kiukweli naomba kumuombea msamaha maana ninafahamu kabisa yupo kwenye wakati mgumu sana na ikumbukwe kwamba naye ni binadamu kwa hiyo mimi na familia yangu tunamuombea ili aweze kupita katika hili.
Mimi ndo Ningekuwa Dogo Janja Ningetembea kwa Mguu Kutoka Dar Hadi Mwanza
0
November 07, 2018
Tags