Mke wa Bilionea Msuya Akiri Kumuua Wifi Yake


IMEELEZWA na upande wa mashtaka katika kesi ya mauaji ya dada wa marehemu bilionea Erasto Msuya, Bi. Aneth Msuya kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa, mshtakiwa namba moja katika kesi hiyo, Miriam Mrita, ambaye ni mjane wa Erasto kuwa alikiri kumuua wifi yake.

Wakili wa Serikali mwandamizi, Patrick Mwita akisaidiana na wakili Faraji Nguka, alitoa maelezo hayo jana wakati akisoma maelezo ya mashahidi katika kesi hiyo ya uchunguzi wa mauaji namba 5 ya mwaka 2017, inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ambapo washtakiwa Mariam na mwenzake Revocatus Muyella, wanaowakilishwa na Peter Kibatala, wanadaiwa kumuua kwa makusudi Aneth kwa kumchinja akiwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, mnamo Mei 25, 2016.

Wakili Nguka alisema mshtakiwa Mariam baada ya kukamatwa, Agosti 7, 2016 alihojiwa na askari Koplo Mwaka, mrakibu msaidizi wa Polisi (ASP) Jumanne na WP Latifa Mohamed na kukiri kuhusika na mauaji hayo na kwamba alimuua wifi yake kutokana na mgogoro wa mali za mumewe (bilionea Msuya ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi Agosti 7, 2013 eneo la Mijohoroni wilayani Hai) na kwamba pia alikuwa na hasira baada ya wifi yake Aneth (Marehemu) kumtumia picha za kumkashifu umbile lake.

Wakili alidai kuwa mshtakiwa alieleza kwamba Aneth alikuwa akimtumia picha zinazoonyesha wanawake wenye maumbile makubwa na mabaya, wenye matumbo makubwa, jambo lililomkasirisha na kuamua kutafuta ushauri kwa Muyella (mshtakiwa wa pili), ambaye alimshauri kumuua.

Washtakiwa wanadaiwa kupanga na kutekeleza mauaji hayo, huku Mariam akimuahidi Muyella kumlipa Tsh milioni 20, kwa kazi hiyo ambapo alimlipa Tsh milioni 10 za awali wakiwa jijini Dar es Salaam na baada ya kutekeleza mauaji hayo anadaiwa alimlipa Tsh milioni 10 nyingine iliyokuwa imebaki jijini Arusha.

Wakili Mwita alitoa maelezo kuwa baada ya kumkamata na kumhoji, Muyella alikubali kumfahamu Mariam kwamba ni mfanyabiashara mwenzake na alikuwa akifahamiana na marehemu mumewe (bilionea Msuya), japo alikana kuhusika na mauaji hayo.

Wakili Mwita alisema mshtakiwa huyo alitambuliwa kwenye gwaride la utambuzi na msichana wa kazi wa marehemu Aneth, Getrude Mafuru ambapo upande wa mashtaka baada kueleza hayo, ulidai kuwa utakuwa na jumla ya mashahidi 45 na vielelezo zaidi ya 14 kwa ajili ya kesi hiyo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad