Mkutano wa Wakuu wa nchi za Afrika Mashariki (EAC) Kufanyika Jijini Arusha Ijumaa Novemba 30

Mkutano wa Wakuu wa nchi za Afrika Mashariki (EAC) Kufanyika Jijini Arusha Ijumaa Novemba 30
Mkutano wa 20  wa wakuu wa nchi za Afrika Mashariki (EAC) unatarajiwa kufanyika Ijumaa Novemba 30, 2018 jijini Arusha.

Mkutano huo umetanguliwa na mkutano wa siku tatu wa baraza la mawaziri ulioanza jana Novemba 25, 2018.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Jumatatu Novemba 26, 2018 na mkuu wa mawasiliano kwa umma wa Sekretariati ya EAC, Richard Owora  inaeleza kuwa miongoni mwa ajenda  za mkutano huo ni kupitisha itifaki mbalimbali.

Pia, kuidhinisha ripoti ya  umoja wa kisiasa ikiwa ni njia ya mpito kufikia shirikisho la kisiasa la Afrika Mashariki, mwelekeo wa haraka wa Sudan Kusini kujiunga EAC na kupitia maombi ya Somalia kujiunga kwenye jumuiya hiyo.

Mkutano huo utapitia ripoti yenye  mapendekezo ya kuona njia za kuchochea uundaji wa magari katika nchi za EAC ili kupunguza uingizaji wa magari kutoka nje pamoja na kuangalia kwa kina sekta ya viwanda vya nguo na ngozi ili kupunguza kuagiza bidhaa hizo.

“Katika mkutano wa kawaida wa wakuu wa nchi uliofanyika Kampala, Uganda Februari 23, 2018,  marais hao waliagiza baraza la mawaziri wa EAC kuchagiza uanzishaji wa kiwanda cha magari  ili kupunguza uagizaji kutoka nje na kuongeza ushindani katika kanda ya EAC,” anaeleza Owora.

Katika hatua nyingine mkutano huo utapitia mapendekezo ya baraza la mawaziri waliopendekeza EAC iwe na naibu makatibu wakuu wawili ambao watapatikana kupitia usaili na nafasi hizo zitakuwa za mzunguko kwa nchi wanachama.

Kwa sasa kila nchi mwanachama ina nafasi ya kuwa na naibu katibu mkuu anayeteuliwa na rais  wa nchi husika kisha jina lake kuidhinishwa na marais wenzake,

Pia mkutano huo utapitisha kuwa sheria miswada mbalimbali ambayo imejadiliwa na kupitishwa na Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) ambayo ni muswada wa kudhibiti bidhaa za nailoni wa mwaka 2016, muswada wa Utawala wa Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) wa mwaka 2018.

Miswada mingine ni kuanzishwa taasisi ya Fedha ya EAC ya mwaka 2018 na muswada wa maboresho ya usimamizi wa forodha wa EAC.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad