Shirikisho la soka nchini (TFF) kupitia kwa Mwenyekiti wa kamati ya Uchaguzi, Malangwe Mchungahela imesema kwamba haimtambui Yussuf Manji kama Mwenyekiti wa Yanga kwani katiba ya timu hiyo hairuhusu mkutano mkuu kumrejesha mwenyekiti aliyejiuzulu.
Hatua hiyo imekuja baada ya jana jioni wajumbe wa kamati ya utendaji ya klabu ya Yanga kukutana na mwenyekiti huyo wa kamati ya uchaguzi wakiwa na hoja ya kukubali kufanya uchaguzi katika nafasi zingine isipokuwa nafasi ya Mwenyekiti.
"Sisi kama TFF hatumtambui Manji kama mwenyekiti wa Yanga maana alishakutana na Waziri wa Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ili kuzungumzia suala la kurudi Yanga na alimkatalia'', alisema Mchungahela.
Mchungahela alisisitiza kwa mujibu wa katiba ya Yanga, Ibara ya 28 kanuni ya tatu (kifungu kidogo c), inasema mjumbe atakoma kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji iwapo atashindwa kutekeleza majukumu ya mjumbe kutokana na kuumwa au sababu nyingine yoyote kwa kipindi cha miezi 12 mfululizo.
Katiba hiyo ya marekebisho ya mwaka 2010, Ibara ya 14 inamruhusu mwanachama yoyote kujiuzulu na kuwasilisha barua kwa katibu mkuu wa Yanga kwa barua ya rejesta. Mchungahela alisema kwa kuzingatia hilo hawamtambui Uenyekiti wa Manji.