Mmiliki wa klabu ya Liverpool John W. Henry amehusishwa na ripoti za kutaka kuiuza klabu hiyo kimya kimya huku taarifa zikisema kwamba yuko tayari kusikiliza ofa za matajiri mbalimbali wanaotaka kuimiliki klabu hiyo.
Bilionea Henry, aliinunua Liverpool kutoka kwa Wamarekani wenzake Tom Hicks na George Gillett mwaka 2010 kwa dola 477 millioni ambazo ni sawa na sh. 1.09 trilioni za kitanzania.
Uwekezaji wake umekuwa mkubwa katika kikosi hicho, kikifanikiwa kufika fainali ya klabu bingwa Ulaya mwezi Mei mwaka huu, pia ikiendelea kutoa changamoto kubwa katika kampeni ya kuusaka ubingwa wa EPL msimu huu. Lakini inaonekana sasa tajiri huyo yuko tayari kuondoa hisa za kampuni yake ya 'Fenway Sports Group' katika klabu hiyo endapo mnunuzi mwenye dau kubwa atapatikana.
Kulingana na ripoti ya mtandao wa 'New York Post', Henry amezindua mchakato wa mauzo. Hiyo ina maana kwamba yeye hajatafuta mnunuzi kikamilifu, hata hivyo inasemekana kuwa 'anatoa ofa kwa faragha' katika kile kinachoelezwa kama kufanya mambo hayo kutokuwa rasmi. Bei ya kuiuza klabu hiyo inasemekana kuwa ni dola 2 bilioni.
Liverpool tayari imehusishwa kutaka kununuliwa na matajiri mbalimbali kutoka Abu Dhabi hasa, Sheikh Khaled Bin Zayed Al Nahayan, binamu wa mmiliki wa Manchester City Sheikh Mansour pamoja na wawekezaji wa China.
Uvumi wa kuuzwa ka klabu hiyo kwa £ 2bn kutoka kwa Sheikh Khaled ulienea hivi karibuni mwezi Agosti, ambapo taarifa hiyo ilikanushwa na uongozi unaomiliki klabu hiyo ukisema kwamba haukuwa na nia yoyote ya kuuza, bali ilifungua milango ya uwekezaji wa nje.