Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuberi ametumia Baraza la Maulid kuwataka Masheikh wa mikoa nchini kukemea vitendo vya ushoga ambavyo vinaharibu sifa ya Uislamu.
Mufti amesema hayo leo Jumanne Novemba 20, 2018 alipokuwa akiwahutubia wananchi katika kumbukizi hiyo ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) inayofanyika kitaifa Wilaya ya Korogwe jijini Tanga.
Amesema jambo la ushoga hapa nchini halikubaliki na linapaswa kupingwa kwa nguvu zote. “Jambo la ushoga halikubaliki, haiwezekani nchi tukufu kama Tanzania kuwa na vitendo hivi, masheikh lisemeeni jambo hili ili tunusuru umma na Taifa kwa ujumla,” amesema.
Baraza hilo limeongozwa na Waziri wa Nchi, Tamisemi Selemani Jafo kwa niaba ya Rais John Magufuli na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na Serikali.