Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu nchini Saudi Arabia imemaliza uchunguzi wake juu ya nani aliyeamuru kuuawa kwa mwanahabari Jamal Khashoggi na kufikia kikomo kuwa haikuwa Mwanamfalme Mohammed bin Salman.
Uchunguzi huo umebaini kuwa mauaji hayo yaliamuriwa na afisa mwandawizi wa idara ya usalama wa taifa ya Saudia ambaye alipewa kazi ya kumshawishi Khashoggi kurejea Saudia. Mwanahabari huyo ambaye alikuwa kinara wa kumkosoa Bin Salman alikimbia Saudia mwaka 2017 na kuhamia Marekani.
Kwa mujibu wa msemaji wa ofisi hiyo, Khashoggi alidungwa sindano ya sumu baada ya purukushani kuibuka ndani ya ofisi ndogo za ubalozi wa nchi hiyo jijini Istanbul, Oktoba 2, 2018.
Mwili wa Khashoggi 'uliyeyushwa kwenye tindikali'
Jamal Khashoggi
Watu 11 tayari wameshafunguliwa mashtaka kutokana na mkasa huo na waendesha mashtaka wanataka watano kati yao kupatiwa adhabu ya kifo. Uchunguzi unaendelea kwa watu wengine 10 ambao wanshukiwa kushiriki mauaji hayo.
Katika mkutano na waandishi wa habari, Naibu Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Saudia Shalaan bin Rajih Shalaan amesema mwili wa Khashoggi ulikatwa katwa ndani ya ubalozi baada ya kuuawa.
Vipande hivyo vya mwili vilikabidhiwa kwa mshirika wao ambaye ni raia wa Uturuki nje ya ubalozi. Tayari picha ya kuchora ya mshirika huyo imetolewa na uchunguzi unaendelea kujua vipande hivyo vya mwili vilipelekwa wapi.
Bwana Shalaan hata hivyo hakuwataja wale ambao wamefunguliwa mashtaka juu ya tukio hilo.
Mwendesha Mashtaka Saudia ataka Waliomuua Mwanahabari Khashoggi Wapatiwe Adhabu ya kifo
0
November 16, 2018
Tags