Askofu wa Kanisa la Kiinjili Kiluteri Tanzania (KKKT), Dayosisi na Mashariki na Pwani, Askofu Alex Malasusa amewataka watu waendelee kumuombea aliyekuwa moja ya waanzilishi wa makampuni ya IPP Mama Mercy Anna Mengi ambaye alifariki dunia Oktoba 31 mwaka huu.
Akizungumza katika ibada maalum ya kuuaga mwili wa marehemu Mama Mercy Anna Mengi ambao ilihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa kitaifa ambapo Askofu Malasusa alinukuu neno la Biblia kutoka Paulo 4 mstari 13 hadi14 na Paulo 5 mstari 1 hadi 2.
“Jambo kubwa na la maana kwetu sisi ni kuwa na uhakika kwa mungu kwa kushika na mapenzi yake, na hata katika hili tuyakubali mapenzi yake kama inavyosema sala yake, ili tuendelee kuishi kwa mapenzi yake,” amesema Dkt Alex Malasusa.
Askofu Malasusa amesema “Mungu ameweka siri kubwa kwenye suala la kifo, hata sisi wachungaji Mungu ametuficha bali ni siri yake yeye mwenyewe Mungu, niwaombe ndugu jamaa tuendelee kujiweka karibu nayeye ili kila mtu afikie tamanio la kwenda mbinguni.”
Miongoni mwa watu walioshiriki ibada hiyo ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli, Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda.
Ibada hiyo iliyofanyika Jijini Dar es salaam, ilianza majira ya saa 6 mchana na kuongozwa na Askofu wa kanisa hilo, Dkt Alex Malasusa akisaidiwa na msaidizi wake Chadiel Luiza.
Mwili wa Mama Mercy Mengi unatarajiwa kusafirishwa kuelekea Machame Moshi kwaajili ya maziko Jumamosi Novemba 10, 2018.
Mama Mercy Anna Mengi atakumbukwa kama moja ya waanzilishi wa makampuni ya IPP ambayo inamiliki vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo EATV, EA Radio, ITV, NIPASHE, The Guardian, Radio One, na Capital Radio.