Baada ya kuwepo kwa tetesi za muda mrefu kuwa mmoja wa wanachama wa muda mrefu wa klabu ya Yanga, Ibrahimu Akilimali, maarufu mzee Akilimali, hatimaye amejitokeza na kuweka wazi sababu za kutojitokea kugombea uongozi ndani ya Yanga.
Kupitia mahojiano maalum na www.eatv.tv, Mzee Akilimali amekiri kuwa alikuwa na nia kubwa ya kuwania nafasi ya Uenyekiti Yanga lakini katiba imemkwamisha kutokana na kukosa baadhi ya vigezo.
''Kiukweli awamu hii nilikuwa nimejipanga kabisa nichukue fomu lakini niliposoma vizuri katiba ya Yanga nikagundua inanipa nafasi ya kugombea ila sasa niliposoma maelekezo ya TFF yananitaka niwe na elimu kuanzia kidato cha 4 na kuendelea na hapo ndipo nikakwama'', amesema.
Aidha amefunguka kuwa pamoja na vigezo hivyo kumweka kando anakiri kuwa elimu yake ya zamani ambayo ni ya darasa la 4 inaizidi kwa kiasi kikubwa elimu ya sasa ya sekondari ila kwasababu katiba inataka hivyo hana budi kukubali.
Mzee huyo amewashauri wapenzi na wanachama wa Yanga kuamini kuwa Yanga itakapomaliza uchaguzi wake Januari 13, 2019 itakuwa bora sana kwani kuna wawekezaji wengi tu wataingia baada ya kuwa na hali ya utulivu.