Kamanda wa Polisi mkoa huo, Suleiman Hassan Suleiman alisema vijana 10 wanaoshikiliwa na jeshi hilo ni kutokana na kutuhumiwa kwa uhalifu na si ushoga.
Alisema polisi hawana ushahidi wowote hadi sasa ambao unaweza kuthibitisha vijana hao kuwa wanajihusisha na vitendo vya ushoga kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.
Kamanda Suleiman alisema vijana hao wamekamatwa baada ya polisi kupata taarifa kutoka kwa wananchi wa kijiji cha Pongwe kuwa wanajihusisha na vitendo vya uhalifu.
Alisema baada ya kupata taarifa hizo polisi walikwenda na kufanikiwa kuwakamata 10 ambao wanatoka maeneo mbalimbali ya Unguja na baadhi walifanikiwa kukimbia.
Alisema hadi sasa wanawashikilia vijana hao kwa ajili ya kuwahoji na iwapo watabainika kuwa na tuhuma zozote watafikishwa kwenye vyombo vya sheria kujibu tuhuma zao.
Kuhusu iwapo jeshi hilo litataka kujiridhisha na madai ya baadhi ya watu wakiwahusisha na vitendo vya ushoga, Kamanda Suleiman alisema polisi hawafanyi kazi kwa matakwa ya watu bali kwa mujibu wa sheria.
Aidha, kamanda huyo alisema wakati jeshi hilo lilipokwenda kwenye maeneo ya fukwe za Pongwe ambazo vijana hao na wenzao walikuwapo hawakuona dalili za kufanya matendo yoyote yale ya ushoga kama inavodaiwa na baadhi ya watu visiwani hapa.
Aliitaka jamii kuepuka kusambaza taarifa zisizokuwa sahihi kwani licha ya kuwachafua wahusika lakini pia zinaichafua Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.