Imeelezwa kwamba tabia ya wazazi kutoa ahadi ya zawadi kwa kila wanachofanya watoto wao ni kibaya na kinawajengea mazingira magumu watoto hao baadae hasa pindi hali ya uchumi inapobadilika.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Arusha Inspekta Happyness Temu wakati alipokuwa anafafanua aina za malezi katika kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa hewani kila siku Asubuhi katika kituo cha Redio cha Triple “A” kilichopo jijini hapa.
Inspekta Happyness alisema kwamba, baadhi ya wazazi wamekuwa na tabia ya kutoa ahadi ya fedha au vitu kwa watoto wao kwa nia ya kutoa hamasa ili wafanye vizuri aidha katika masomo au shughuli zozote hali ambayo kimalezi si sahihi kwani inaweza kusababisha mtu kuwa tabia tofauti pindi atakapokuwa mkubwa.
“Tabia hii inawafanya watoto wanapokuwa kwenye malezi wawe na matumaini kwamba kila kizuri wanachofanya lazima mwishoni kiendana na zawadi na hivyo mtoto anasababishiwa tamaa, mfano ukimaliza ugali wote nakununulia keki”. Alisema Inspekta Happyness.
Alisema pindi anapokuwa mtu mzima hali hiyo itamuathiri kwa kuwa atakuwa anataka kupewa asante ya kitu au fedha kutoka kwa kila atayemhudumia mara baada ya kumaliza kazi kitu ambacho si sahihi.
Alisema pongezi kwa mtoto sio lazima iendane na kuahidiwa na kupewa kitu au fedha bali inaweza kufanyika kwa njia ya maneno tu na ikamridhisha kwani si kila wakati mzazi unaweza ukawa na uwezo ule ule kiuchumi kuna wakati unashuka au mtoto anakuwa mikononi mwa walezi wengine ambao uwezo wao ni mdogo.
Akifafanua juu ya aina ya malezi alisema kwamba yapo ya aina tatu ambayo ni malezi ya kimabavu; ambapo mzazi au mlezi anaweka sheria ambazo atataka zifuatwe bila kutoa nafasi ya kumsikiliza mtoto.
“Hali hii inasababisha mtoto asiweze kuwa na mazingira huru ya kujifunza kitu chochote kipya zaidi ya kile atakachoelekezwa katika mazingira ya ndani kwa kuwa atakuwa anaogopa kugusa hata Redio au TV, lakini pia anakosa kujiamini na wakati mwingine analazimika kuwa muongo pindi anapokwenda kinyume kwa kuogopa kupata kipigo”. Alifafanua Inspekta Happyness.
Alisema aina ya pili ni malezi ya Kidemokrasia ambapo wazazi hutumia muda mwingi kujenga mahusiano kwa watoto wao lakini pia wanaweka sheria na kuwaambia faida zake kama zitafuatwa na hasara zake kama zitavunjwa.
“Watoto wanaolelewa katika hatua hii wanakuwa na uthubutu wa kufanya jambo jema lakini pia huwa wanakuwa na uwezo wa kutathmini zuri na baya na kisha kufanya maamuzi sahihi”. Alisema Inspekta Happyness.
Aidha alisema kwamba aina ya tatu ni malezi huru ambapo wazazi wanaweka sheria kwa watoto wao lakini hawazifuatilii hivyo wanatoa mwanya mkubwa kwa watoto kuwa huru zaidi.
Katika hatua hii watoto wanaweza kujiingiza katika makundi mabaya bila hata mzazi kujua kwa kuwa anakuwa mbali nao na ni rahisi kumtetea mtoto wake kwa lolote baya kwa kuwa hajawahi kumshuhudia au kusikia.
Jeshi la Polisi mkoani hapa kupitia Dawati la Jinsia na Watoto limekuwa likitoa elimu juu ya vitendo vya unyanyasaji na ukatili kupitia mikutano ya hadhara, nyumba za Ibada na Redio mbalimbali kwa lengo la kuwaelimisha wananchi ili washiriki moja kwa moja kutoa taarifa na kusaidia kutokomeza vitendo hivyo.