Rais John Magufuli ametoa dola za Marekani 20,000 ambazo ni wastani wa Sh50 milioni ili kuchangia matibabu ya Mkurugenzi wa vipindi wa Clouds Media group, Ruge Mutahaba.
Ruge ambaye alianza kusumbuliwa na ugonjwa ambao bado haujawekwa wazi tangu mwanzoni mwa mwaka huu anapatiwa matibabu Afrika Kusini.
Akizungumza leo katika kipindi cha Clouds 360 kinachorushwa na televisheni ya Clouds, Mkuu wa Vipindi wa redio hiyo, mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo, Sebastian Maganga amesema hatua hiyo ya Rais imefikiwa baada ya kusikia Ruge anaumwa kwa muda na zilimsikitisha.
“Aliamua kumshika mkono kama baba afanyavyo kwa mwana wa kumzaa, kumshirikisha katika maombi na alinyoosha mkono kwetu akituambia changamoto za kiafya ni kubwa na la awali ambalo anataka kulifanya ni kuchangia mfuko wa kiafya na changamoto zisiwe gharama za kimatibabu,” amesema Maganga akinukuu maneno ya Rais Magufuli.
Mbali na Rais kutoa mchango wa matibabu pia Maganga amebainisha kuwa wameamua kuweka wazi juu ya afya ya Ruge kutokana na kuwepo kwa maneno mengi katika mitandao ya kijamii.
“Yalizungumzwa mengi na sisi tuliona wakati haukuwa mzuri sana kuzungumza na tuliona tukifanya yoyote tutaleta maswali mengi ambayo hata yeye hakupenda,”
"Katikati ya Mei kulelekea Juni hali ya Mkurugenzi haikuwa nzuri akatuomba kupata muda kidogo ili ashughulikie afya yake tuliona hili litakuwa dogo tu na tukatoa baraka zote,”
“Lakini ripoti za kitabibu zikasema muda wa kupumzika ni mdogo hivyo akaongezewa muda na katikati ya Juni na Julai alirejea na kasi ya kawaida kwenye kazi na wiki mbili tatu tukawa naye na hapo ndiyo tulikuwa tunakaribia kuanza Tigo Fiesta Moro,”
“Akatuambia anabidi aelekee kwenye taratibu za kimatibabu na nikiri bado changamoto hizo zipo na madaktari wanakiri Kiongozi wetu ni mpambanaji na bado anahitaji muda wa kupumzika na ni kweli hizo changamoto zilikuwepo" amesema Maganga na kuongeza kuwa
“Tunashukuru mara nyingi ukipata changamoto A ya kiafya changamoto B inajitokeza na tunashukuru taratibu hali yake inarudi na kuna hatua kubwa ya kimaendeleo."
Rais Magufuli Achangia Milioni 50 ya Matibabu ya Ruge Mutahaba
0
November 20, 2018
Tags