Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ameshiriki ibada ya kuuaga mwili wa aliyekuwa Askofu Kanisa Katoliki wa Jimbo la Mbeya, Askofu Evarist Chengula na kusema kiongozi huyo alikuwa moja ya watu mahiri nchini
Akizungumza kwenye ibada takatifu iliyofanyika kanisa la Mtakatifu Immaculata Kurasini Jijini Dar es salaam, Rais Magufuli amesema Askofu Chengula alikuwa moja ya viongozi wa dini wa mfano waliopinga hadharani vitendo vya mapenzi ya jinsia moja.
“Askofu Chengula ameitangaza injili kwelikweli, hakusita kuzungumza ukweli na hivi karibuni alizungumza na kupinga hadharani kuhusu ushoga, ni viongozi wachache wanaoweza kupinga hadharani maovu yaliyokatazwa kwenye biblia.”
“Kwa nafasi hii nawapa pole sana waumini wa Kanisa Katoliki na watu wake wa Jimbo la Mbeya, na Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya marehemu mahali pema peponi amina,” ameongeza Rais Magufuli.
Novemba 21 mwaka huu Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbeya, Evarist Chengula alifariki dunia majira asubuhi akiwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete alipokuwa anapatiwa matibabu ya moyo.