Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Magufuli Apongezwa kwa Kuwezesha Wanyonge
0
November 18, 2018
Frank Mvungi- MAELEZO, Njombe
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amepongezwa kwa kuendelea kuwawezesha wajasiriamali kupitia Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) .
Akizungumza wakati akifunga mafunzo ya siku 10 kwa wajasiriamali zaidi ya 700 wa Mjini Njombe Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Christopher Ole Sendeka amesema kuwa swala la urasimishaji Biashara kwa wajasiriamali ni takwa la Kisheria na pia ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ibara ya 58 ambapo Biashara zote zinatakiwa kuendeshwa katika mfumo rasmi na Serikali ya Awamu ya Tano imeweka mkazo mkubwa ili kuwainua wajasiriamali wanyonge.
“ Nawapongeza MKURABITA na Halmashauri ya Mji wa Njombe kwa kufanikisha mafunzo haya kwa wajasiriamali yanayolenga kuwajengea uwezo ili waweze kurasimisha Biashara zao na pia kuanzishwa kwa Kituo Kimoja cha Urasimishaji Biashara hapa Njombe itakuwa ukombozi kwa wajasiriamali wetu”; Alisisitiza Ole Sendeka.
Akifafanua Mhe. Ole Sendeka amesema kuwa kuanzishwa kwa Kituo cha Urasimishaji na Uendelezaji wa Biashara Mjini Njombe kumewashirikisha wadau kama MKURABITA, TRA, SIDO na Benki mbalimbali ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kukabiliana na tatizo la Ongezeko la Biashara ndogo na za kati zisizo rasmi na ambazo zinakuwa kwa kasi.
Aliongeza kuwa wananchi wote wanajukumu kubwa la kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto zilizopo katika maeneo yao hasa kwa wajasiriamali kuhakikisha kuwa wanatoa taarifa za wale wote wanaotaka kukwamisha juhudi za Serikali zinazolenga kuwainua.
Kwa upande wake Mratibu wa MKURABITA Bi. Seraphia Mgembe amesema kuwa washiriki wa mafunzo hayo wamejengewa uwezo katika maeneo yafuatayo; Urasimishaji na Usajili wa majina ya Biashara, Upatikanaji wa leseni za Biashara na faida zake, utunzaji wa kumbukumbu za Biashara na umuhimu wake, huduma kwa mlipa kodi, Huduma za mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Mbinu za Masoko.
Aliongeza kuwa wajasiriamali wakirasimisha Biashara zao watakuza mitaji yao na kupanua masoko kwa kuwa watakuwa na uwezo wa kukopa katika Taasisi za fedha yakiwemo mabenki.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi. Ruth Msafiri amesema kuwa wajasiriamali wanapaswa kujenga utamaduni wa kurejesha kwa wakati mikopo wanayokopa katika kupitia Taasisi za fedha ili waweze kukuza Biashara zao.
Pia alishauri Halmashuri kuangalia namna Bora yakuwawezesha wajasiriamali wanaoanza Biashra ili kuweka utaratibu utakaosaidia kukuza Biashara zao.
Mafunzo yakuwajengea uwezo wajasiriamali yamefanyika Mkoani Njombe yakilenga kuwajengea uwezo ili waweze kurasimisha biashara zao na kuchangia katika kukuza uchumi. Wajasiriamali zaidi ya 700 wameshiriki katika mafunzo hayo ya siku 10.
Tags